Larijani: Chaguo la kijeshi haliwezi kusuluhisha mgogoro wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56611-larijani_chaguo_la_kijeshi_haliwezi_kusuluhisha_mgogoro_wa_syria
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mgogoro wa Syria hauwezi kupatiwa ufumbuzi kupitia uingiliaji wa kijeshi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2019 04:31 UTC
  • Larijani: Chaguo la kijeshi haliwezi kusuluhisha mgogoro wa Syria

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema mgogoro wa Syria hauwezi kupatiwa ufumbuzi kupitia uingiliaji wa kijeshi.

Ali Larijani amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mazungumzo yake na mwenzake wa Algeria, Slimane Chenine mjini Belgrade, Serbia wanakoshiriki mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU).

Spika Larijani amebainisha kuwa, "Hata kabla ya kuanza vita katika nchi za Yemen na Syria, Jamhuri ya Kiislamu ilitoa pendekezo la kupewa kipaumbele chaguo la mazungumzo kwenye migogoro ya nchi hizo, lakini baadhi ya nchi zilikhiari na kushinikiza chaguo la kutumia nguvu za kijeshi."

Dakta Ali Larijani amesisitiza kuwa, mgogoro wa Syria hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa nguvu za kijeshi, na chaguo bora la kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Kiarabu ni mazungumzo.

Magari ya deraya ya Uturuki kaskazini mwa Syria

Hii ni katika hali ambayo, taasisi mbalimbali za kimataifa zimeendelea kulaani operesheni ya kijeshi inayofanywa na jeshi la Uturuki huko kaskazini mwa Syria kwa siku kadhaa sasa.

Wizara ya Ulinzi ya Uturuki imedai kuwa wanamgambo wa Kikurdi zaidi ya 400 wameuliwa hadi sasa tangu kuanza oparesheni hiyo iliyopewa jina la "Chemchemi ya Amani". Rais Recep Tayyep  Erdogan wa Uturuki anasisitiza kuwa operesheni hiyo itaendelea licha ya vitisho vya kuwekewa vikwazo vya Marekani na nchi za Ulaya.