Uturuki: Amani hatarini baada ya Marekani kumuua Lt. Jen. Soleimani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema hatua ya Marekani kumuua kamanda Luteni Jenerali Qassem Soleimani wa Iran ni kitendo ambacho kitahatarisha amani katika eneo.
Akizungumza Jumatatu mjini Ankara, Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema: "Kuuawa Soleimani ni hatari kubwa kwa amani katika eneo."
Amesema Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefanya mazungumzo ya simu na Rais Hassan Rouhani wa Iran, na pia Marais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Bahram Salih wa Uturuki na Amir wa Qatar Tamim bin Hamad Al Thani kuhusu mauaji hayo. Aidha Erdogan anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuhusu kadhia hiyo. Hali kadhalika Rais Vladimir Putin wa Russia anatazamiwa kuitembelea Uturuki Jumatano kufanya mazungumzo na Erdogan kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo. Katika mahojiano na CNN Turk, Erdogan amesema anaamini kuwa, "kuuawa kamanda wa ngazi za juu wa nchi ni jambo lisiloweza kubakia pasina kujibiwa."
Erdogan amesema ameshangazwa na mauaji hayo, kwani yamejiri masaa machache tu baada ya mazungumzo yake ya simu na Rais Trump wa Marekani ambapo alimtaka achukue hatua za kupunguza taharuki na Iran.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo. Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine wanane, walishambuliwa tokea angani na wanajeshi vamizi na wa kigaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wote wakafa shahidi katika tukio hilo.