London: Kuna washukiwa wa ugaidi 3000 nchini Uingereza
Mkuu wa Jeshi la Polisi la Kupambana na Ugaidi nchini Uingereza amesema kuwa uwepo wa washukiwa 3000 wa hujuma za kigaidi nchini humo, unatia wasi wasi mkubwa.
Neil Basu aliyasema hayo Alhamisi ya jana ambapo sambamba na kuonyesha wasi wasi wake kutokana na uwepo wa karibu watu 3000 wanaoshukiwa kutenda vitendo vya ugaidi nchini humo amesema kuwa, kuwafuta watu hao ni jambo gumu sana. Akibainisha kwamba washukiwa hao wa ugaidi wanafuatiliwa nyendo zao na polisi na kwamba ni suala gumu kuwafuatilia wote kikamilifu, ameongeza kuwa idadi ya watu waliofungwa kutokana na kujishughulisha na vitendo vya kigaidi wamemaliza vifungo vyao na taratibu wataanza kuachiliwa huru.

Baada ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kushindwa nchini Iraq na Syria, idadi ya raia wa nchi za Magharibi waliojiunga na kundi hilo, walirejea nchi zao na hii leo Uingereza inakabiliwa na tatizo la mashambulizi ya kigaidi na wasi wasi wa usalama wake. Kwa mujibu wa ripoti rasmi zilizoenezwa nchini Uingereza, katika kipindi cha karibu miaka miwili ya hivi karibuni nchi hiyo imekumbwa na mashambulizi manane ya kigaidi katika miji tofauti ya nchi hiyo hususan London. Katika hujuma hizo watu 39 wameuawa na wengine zaidi ya 270 kujeruhiwa. Aidha vyombo vya habari vya Uingereza vimetangaza kwamba zaidi ya raia 8000 kutoka nchi za Ulaya, walijiunga na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Iraq na Syria ambapo kurejea kwao katika nchi zao kumewatia tumbo joto viongozi na jamii za mataifa hayo.