Hillary Clinton: Rais Trump ni hatari kwa demokrasia ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59378-hillary_clinton_rais_trump_ni_hatari_kwa_demokrasia_ya_marekani
Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amemtaja Rais Donald Trump wa nchi hiyo kama mtu hatari kwa demokrasia na kusisitiza kuwa, yuko tayari kumuunga mgombea yoyote atakayechuana na mwanasiasa huyo wa Republican katika uchaguzi ujao nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2020 04:32 UTC
  • Hillary Clinton: Rais Trump ni hatari kwa demokrasia ya Marekani

Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amemtaja Rais Donald Trump wa nchi hiyo kama mtu hatari kwa demokrasia na kusisitiza kuwa, yuko tayari kumuunga mgombea yoyote atakayechuana na mwanasiasa huyo wa Republican katika uchaguzi ujao nchini humo.

Hillary Clinton ambaye alichuana na Donald Trump katika kinyang’anyiro cha urais nchini Marekani mwaka 2016 akipeperusha bendera ya chama cha Democrat na kushindwa amesema, "nitamuunga mkono mgombea yeyote wa chama chetu atakayeteuliwa. Ni wazi kuwa Trump ni hatari kwa demokrasia na mustakabali wa Marekani."

Ameeleza bayana kuwa, "hakuna mtu anayempenda (Trump), hakuna anayetaka kufanya kazi naye. Hakuna chochote alichokifanya."

Rais  Donald Trump wa US

Clinton ametoa mwito kwa wananchi wa Marekani wakabiliane na kile alichokiita “mielekeo ya kidikteta” ya Rais Donald Trump na kwamba Trump ni mchochezi na hawezi kujidhibiti.

Waziri huyo wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ambaye amekuwa akimkosoa vikali Trump amewahi kunukuliwa pia akisema kwamba, Donald Trump ndiye rais hatari zaidi katika historia ya nchi hiyo.