Njama za Trump za kuficha sera za Marekani dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59502-njama_za_trump_za_kuficha_sera_za_marekani_dhidi_ya_iran
Baada ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA mwezi Mei 2018, ilianzisha sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran; na katika fremu hiyo ikaiwekea Iran vikwazo vikali kabisa hata katika uga wa masuala ya kibinadamu. Pamoja na kuwepo sera hiyo ya White House, hivi sasa rais afriti wa Marekani anajifanya mtu mwenye kuwahurumia wananchi wa Iran na kudai eti yuko tayari kuisaidia Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 02, 2020 07:29 UTC
  • Njama za Trump za kuficha sera za Marekani dhidi ya Iran

Baada ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA mwezi Mei 2018, ilianzisha sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran; na katika fremu hiyo ikaiwekea Iran vikwazo vikali kabisa hata katika uga wa masuala ya kibinadamu. Pamoja na kuwepo sera hiyo ya White House, hivi sasa rais afriti wa Marekani anajifanya mtu mwenye kuwahurumia wananchi wa Iran na kudai eti yuko tayari kuisaidia Iran.

Siku ya Jumamosi 29 Februari, Trump alitangaza kuwa tayari kuisaidia Iran katika kukabiliana na kirusi cha Corona. Akizungumza katika Kongamano la Harakati za Kisiasa za Wahafidhina Marekani (CPAC), Trump alidai kuwa: "Sisi tunaweza kuisaidia Iran kukabiliana na kirusi cha Corona. Kile pekee kinachohitajika ni wakuu wa Tehran watuombe msaada."

Trump aliendelea kudai kuwa: "Sisi tuna wataalamu bora zaidi duniani na  tuna hamu ya kuwasaidia Wairani katika kukabiliana na kirusi cha Corona lakini hilo linahitaji kwanza wao watuombe msaada." Trump aliongeza kuwa: "Sisi tumepiga marufuku mtu yeyote kuingia Marekani iwapo amesafiri nchini Iran katika kipindi cha wiki mbili zilizopita."

Trump alikuwa anaashiria marufuku iliyotolewa na makamu wake, Mike Pence, ambaye tarehe 29 Februari alitangaza kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kuingia Marekani iwapo amesafiri nchini Iran katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Amri hiyo ya Marekani imetolewa katika hali ambayo hakuna marufuku ya kuingia Marekani kwa watu waliotembelea nchi ambazo zina idadi kubwa ya watu wanaougua Corona zaidi ya Iran kama vile China, Korea Kusini, Japan na Italia. 

Trump anadai kuwa yuko tayari kuisaidia Iran kukabiliana na virusi vya Corona katika hali ambayo vikwazo vya pande zote na vya kidhalimu vya serikali yake vimepelekea watu wa Iran wawe chini ya mashinikizo makubwa.

Elizabeth Warren, seneta wa jimbo la Massachusetts ambaye pia anawania kupata tiketi ya chama cha upinzani cha Democrats katika uchaguzi wa rais wa Marekani amekiri kuwa, vikwazo vya nchi yake dhidi ya Iran vimepelekea wagonjwa Wairani kupata mashinikizo makubwa na jambo hilo limeathiri vita dhidi ya kirusi cha Corona.

Serikali ya Trump imezidisha mashinikizo dhidi ya serikali kwa lengo la kuilazimisha Iran isalimu amri mbele ya matakwa yake yaliyo kinyume cha sheria na ya kujitakia makuu. Mara kwa mara Marekani hutangaza vikwazo vipya dhidi ya wakuu wa Iran na pia sekta mbali mbali za kiuchumi za nchi hii kiasi kwamba sasa hakuna watu au sekta zilizobakia kwa ajili ya kuwekewa vikwazo. 

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anasema hivi kuhusu nukta hii: "Rais wa Marekani anazungumza kuhusu 'vita vya kiuchumi' lakini sisi tunasema hatua hizo zake ni ugaidi wa kiuchumi kwani anawalenga wananchi wa kawaida."

Marekani imefika mbali zaidi na hata imeweka kando madai yake ya kidhahiri kuhusu kuzingatia masuala ya kibinadamu katika vikwazo na sasa inashadidisha wazi wazi mashinikizo dhidi ya watu wa Iran kwa kuweka vizingiti katika kuingizwa dawa na chakula nchini.

Moja ya nukta ya wazi iliyo dhidi ya ubinadmau katika vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kuweka vizingiti ili kuwazuia Wairani kupata dawa muhimu na za kuokoa maisha hasa dawa zinazohitajiwa na wagonjwa wanaougua magonjwa maalumu na yaliyo thakili. Kwa mujibu wa tovuti ya SRF ya Shirika la Utangazaji la  Uswisi, kwa vikwazo vyake dhidi ya Iran, Marekani imelenga sekta zote za mabadilishano ya kibiashara Iran na jambo hilo limepelekea kuwepo uhaba wa baadhi ya dawa na vyakula nchini Iran na hivyo kuhatarisha maisha ya idadi kubwa ya watu hasa wagonjwa wa saratani.

Hivi sasa, wakati ambao utendaji wa kijinai wa Trump mbele ya taifa la kimapambano la Iran uko wazi, anadai kuwa anataka kuwasaidia Wairani katika kukabiliana na ugonjwa wa Corona; madai ambayo yanatolewa tu kwa ajili ya kupotosha fikra za walimwengu kwa kuonyesha taswira bandia ya ubinadamu ya utawala wa Trump.