ICC yaamuru uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Marekani nchini Afghanistan
Majaji waandamizi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wameamuru uchunguzi uanze kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu ambazo zinaripotiwa kufanywa na askari wa Marekani nchini Afghanistan.
Uamuzi mahakama hiyo yenye makao yake The Hague Uholanzi, unatazamiwa kuikasirisha serikali ya Marekani ambayo ililaani vikali ombi la Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda ambaye alitaka kufanyike uchunguzi kuhusu jinai za askari wa Marekani nchini Afghanistan.
Mwezi Aprili mwaka jana majaji wa ICC walikataa kuruhusu uchunguzi wa uhalifu kama huo katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita kwa madai kuwa Marekani haitatoa ushirikiano unaotakiwa.
Marekani, ambayo sio mwanachama wa ICC, ilitangaza vikwazo vya kipekee dhidi ya mahakama hiyo ya kimataifa, na kumyima visa afisa yeyote "anayehusika moja kwa moja" katika uchunguzi " dhidi ya wanajeshi wa Marekani."
Mwendesha mashtaka Fatou Bensouda alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji mnamo mwezi Septemba. Katika uamuzi wao leo Alhamisi, majaji wa rufaa katika ICC wamesema majaji wenzao katika mahakama ya chini walifasiri vibaya kanuni za ICC wakati walipokataa Marekani ishtakiwe na kwa msingi huo wamesema uchunguzi unapaswa kuendelea.
Marekani iliivamia ardhi ya Afghanistan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha amani nchini humo. Hata hivyo tangu wakati huo Washington imeshindwa kutekeleza ahadi yake, na kinyume chake, hali ya ukosefu wa amani, ugaidi na uzalishaji wa dawa za kulevya vimeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini Afghanistan. Aidha wanajeshi wa Marekani wanalaumiwa kwa kufanya mauaji ya maelefu ya raia wasio na hatia nchini Afghanistan mbali na jinai zingine nyingi nchini humo.