Jumanne Kuu na mustakbali wa uchaguzi wa Wademocrat nchini Marekani
Siku muhimu zaidi katika kalenda ya uchaguzi wa mchujo wa urais wa Marekani ambayo imepewa jina la Jumanne Kuu katika kambi ya chama cha Democrats imemalizika kwa ushindi wa Joe Biden ambaye inaonekana ndiye atakayekabidhiwa bendera ya chama hiyo kwa ajili ya kupambana na Donald Trump katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka huu wa 2020.
Jumanne hiyo, makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden alipata kura nyingi katika majimbo mengi ya nchi hiyo na kumshinda mpinzani wake Seneta Bernie Sanders ambaye kabla ya siku ya Jumanne, alikuwa amempiga kikumbo kikali Biden katika baadhi ya majimbo. Baada ya Sanders aliyeshika nafasi ya pili, Bi Elizabeth Ann Warren alishika nafasi ya tatu huku nafasi ya nne katika uchaguzi huo wa mchujo ikishikwa na bilionea Michael Bloomberg. Wagombea hao wawili wa mwisho katika uchaguzi huo walitupwa mbali kwa wingi wa kura katika zoezi hilo.
Inaonekana kuwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho atakuwa ni Joe Biden ingawa baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, si jambo lililo mbali kumuona Sanders akimpiku tena mpinzani wake Joe Biden kama ilivyokuwa kabla ya Jumanne Kuu. Vile vile kuna kauli kwamba huenda mgombea yoyote kati ya hao asipate akidi inayotakiwa ya kura 1991 za wajumbe maalumu wa chama cha Democrat na hivyo huenda matokeo ya mwisho yasitoe mshindi wa kuweza kukiwakilisha chama hicho katika kinyang'anyiro kijacho cha urais wa Marekani cha tarehe 3 Novemba mwaka huu wa 2020. Wachambuzi wengi wa mambo wanasema kuwa, sehemu kubwa ya wajumbe hao maalumu ambao ni kutoka safu za vigogo wa kisiasa na kichama watampigia kura Joe Biden, makamu wa zamani wa rais wa Marekani na hivyo kumuweka pembe Bernie Sanders, seneta mwenye misimamo ya mrengo wa kushoto ambaye ni mkosoaji mkubwa wa mfumo wa hivi sasa wa kisiasa wa Marekani.
Kiujumla ni kwamba mzunguko wa hivi sasa wa uchaguzi wa mchujo cha chama cha Democrats huko Marekani umekuwa na mambo kadhaa ya kuzingatia. Mosi ni kwamba fedha za bilionea Michael Bloomberg ambaye alichofanya kikubwa ni kumwaga fedha nyingi za kuvutia wapiga kura, hazikumsaidia kitu na amekuwa wa mwisho katika zoezi la upigaji kura la Jumanne Kuu. Jengine ni kwamba, uungaji mkono wa vigogo wote wakuu wa chama cha Democrats umeshindwa kufyeka magugu katika njia ya Joe Biden ya kutimiza ndoto yake ya kuwa mgombea wa urais nchini Marekani. Kinyume na walivyotarajia vigogo hao, uungaji mkono wao huo mkubwa umeshindwa kumsafishia njia wala kumpa ushindi wa mteremko makamu wa zamani wa rais wa Marekani, Joe Biden. Vile vile kampeni kubwa mbaya dhidi ya Sanders kama madai kuwa yeye ni msoshalisti, mpenda mapinduzi bali hata mtu anayewachukia Mayahudi, zimeshindwa kumpunguzia umaarufu wake kiasi kwamba amefanikiwa kumpiga kikumbo Joe Biden katika baadhi ya majimbo muhimu ya Marekani.
Inaonekana wazi kwamba katika siku zijazo tutashuhudia mchuano mkali zaidi baina ya kambi mbili kuu za chama cha Democrats, ile ya wahafidhina inayoongozwa na Joe Biden na ile ya mrengo wa kushoto inayopenda mageuzi chini ya bendera inayopeperushwa na Bernie Sanders ndani ya chama hicho. Viongozi wa chama cha Democrats wana wasiwasi kwamba kaulimbiu na ahadi zinazotolea na Sanders zinaweza kuvuruga utulivu wa kisiasa ndani ya chama na Marekani kiujumla na kuzusha wimbi kubwa la uasi wa kifikra wa watu waliochoshwa na hali mbaya iliyopo Marekani hivi sasa. Wasiwasi wa viongozi hao ni mkubwa kiasi kwamba hata wako tayari kukubali kushindwa na Donald Trump katika uchaguzi ujao kuliko kuruhusu Bernie Sanders kuingia katika Ikulu ya White House.
Alaakullihaal, matokeo ya uchaguzi wa tarehe 3 Machi 2020 ndani ya chama cha Democrats umeonesha kuwa si jambo jepesi kumshinda Bernie Sanders na inabidi kazi kubwa zaidi ifanyike kama viongozi wa chama cha Democrats wanataka Joe Biden abebe rasmi bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa rais wa Marekani wa Novemba 3, 2020.