Mar 21, 2020 01:33 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN atuma ujumbe kwa munasaba wa Nowruz

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za kheri na fanaka kwa munasaba wa kuwadia siku kuu ya Nowruz (Nairuzi) ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia na wakati huo huo akatuma salamu za rambi rambi kutokana na kupoteza maisha idadi kubwa ya watu kutokana na ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Katika salamu zake hizo kwa munasaba wa Nowruz, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea matumaini yake kuwa, pamoja na kuwepo majonzi yaliyoenea kote kutokana na corona, siku kuu ya Nowruz itaweza kuwaletea wanaadamu furaha.

Katika ujumbe wake huo  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Mwaka huu, sherehe za Nowruz zinaanza wakati wa majonzi na masikitiko. Ugonjwa wa COVID-19 umeenea duniani kote ikiwa ni pamoja na maeneo yanayoadhimisha sherehe hii kongwe."

Gutteres amesema, 'Kila mwaka huwa tunaadhimisha Nowruz kama siku ya mwanzo mpya, wakati tunapoingia katika mwaka mpya kwa matumaini na furaha. Sisi huadhimisha kuhuishwa tena mazingira na pia tunaadhimisha siku ya kwanza ya msimu wa machipuo."

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, watu wasiopungua 255,000 wameambukizwa ugonjwa wa COVID-19 kote duniani na miongoni mwao zaidi ya 10,000 wameaga dunia.

 

Tags