China yaishangaa Marekani kutaka kulipwa fidia ya Corona
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60608-china_yaishangaa_marekani_kutaka_kulipwa_fidia_ya_corona
China imesema madai ya Marekani kwamba serikali ya Beijing ilishindwa kushughulikia ipasavyo mlipuko wa virusi vya Corona si sahihi na hayana misingi yote ya kisheria, na kwamba takwa la taifa hilo la kutaka kulipwa fidia na China kutokana na madhara ya virusi hivyo si chochote ghairi ya tamthilia ya kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2020 03:21 UTC
  • China yaishangaa Marekani kutaka kulipwa fidia ya Corona

China imesema madai ya Marekani kwamba serikali ya Beijing ilishindwa kushughulikia ipasavyo mlipuko wa virusi vya Corona si sahihi na hayana misingi yote ya kisheria, na kwamba takwa la taifa hilo la kutaka kulipwa fidia na China kutokana na madhara ya virusi hivyo si chochote ghairi ya tamthilia ya kisiasa.

Katika makala iliyochapishwa jana Jumamosi na Shirika la Utangazaji la China (CMG), Beijing imeashiria hatua ya serikali kadhaa za majimbo ya Marekani ya kuwasilisha mafaili mahakamani, zikitaka kulipwa fidia na China, kwa madai kuwa ugonjwa wa Covid-19 ulianzia katika nchi hiyo ya Asia.

Shirika hilo la China Media Group limeandika: Kesi hizo zimewasilishwa mahakamani kwa lengo la kuficha mapungufu na uzembe wa Washington katika kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona nchini Marekani.

Wiki hii, Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Missouri, Eric Schmitt pamoja na mwenzake wa Mississippi, Lynn Fitch walifungua kesi katika mahakama za majimbo hayo dhidi ya China, wakiituhumu Beijing kuwa ilishughulikia visivyo mlipuko wa Corona, hatua ambayo eti imezisababishia hasara kubwa chumi za majimbo hayo.

Katika sehemu moja ya makala hiyo ya jana Jumamosi, Shirika la Utangazaji la China limesema, "tangu mlipuko wa Corona uanze, wanasiasa wachache walaghai mjini Washington, wamekuwa na uchu mkubwa wa kulitumia janga hilo kwa ajili ya maslahi yao ya kisiasa."

Watu zaidi ya 52,000 wamekufa kwa Corona US, nchi hiyo inaongoza kwa idadi ya vifo na mambukizi duniani

Watu zaidi ya 52,000 wameaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini Marekani huku walioambukizwa virusi hivyo wakikaribia milioni moja, na hivyo kuifanya nchi hiyo iwe muathirika mkubwa zaidi wa janga la Corona duniani.

Itakumbukwa kuwa, baada ya kuenea virusi hivyo nchini Marekani na kuongezeka mashinikizo dhidi yake, Rais Donald Trump alilituhumu Shirika la Afya Dunia WHO kwamba linaipendelea China na baadaye akalikatia shirika hilo misaada. Aidha anaituhumu serikali ya Beijing kuwa imezalisha virusi hivyo katika maabara na kuitaja China kuwa chanzo cha mlipuko wa maambukizi ya virusi hivyo duniani, madai ambayo si tu yamekabidhishwa na China, bali pia na WHO.