Marekani yaiwekea Huawei vikwazo vipya, uhusiano na China wazidi kuharibika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61010-marekani_yaiwekea_huawei_vikwazo_vipya_uhusiano_na_china_wazidi_kuharibika
Serikali ya Marekani imeliwekea vikwazo vipya shirika kubwa la kiteknolojia la China Huawei na hivyo kupelekea uhusiano wake na China ambao umezorota kuwa mbaya zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 16, 2020 03:09 UTC
  • Marekani yaiwekea Huawei vikwazo vipya, uhusiano na China wazidi kuharibika

Serikali ya Marekani imeliwekea vikwazo vipya shirika kubwa la kiteknolojia la China Huawei na hivyo kupelekea uhusiano wake na China ambao umezorota kuwa mbaya zaidi.

Waziri wa Biashara wa Marekani Wilbur Ross Ijumaa alitangaza kuwa hatua hiyo itaizuia Huawei kutumia teknolojia ya Marekani kuunda kifaa kinachojulikana kama semiconductor.

Amedai kuwa Huawei imekuwa ikitumia mwanya wa kisheria katika kutumia teknolojia ya Marekani kuunda kifaa hicho lakini sasa haitawezekana tena.

Marekani inasema kifaa hicho ambacho huundwa katika nchi za nje kimekuwa kikiuziwa shirika la Huawei. Sheria mpya ya vikwazo inazuia shirika lolote kuiuzuia Huawei kifaa hicho iwapo utengenezaji wake umetumia teknolojia ya Marekani.

China imetoa radiamali ya haraka na kusema itachukua hatua dhidi ya mashirika ya Marekani. Kati ya hatua hizo ni kuyawekea vizingiti mashirika ya Marekani kama vile Apple, Cisco Systems na Qualcomm pamoja na kusitisha ununuzi wa ndege za Boeing za Marekani.

Rais Trump wa Marekani amechukua hatua kadhaa dhidi ya Huawei

Serikali ya Trump na kwa visingizio tofauti vikiwemo vitisho vya kiusalama, imekuwa ikishadidisha mashinikizo dhidi ya washirika wake likiwemo Shirika la Huawei ambalo ni shirika kubwa la mawasiliano la China, kuuza bidhaa zake ndani ya taifa hilo. Hii ni katika hali ambayo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kwamba shirika hilo la mawasiliano la Huawei linaisaidia serikali ya Beijing kufanya ujasusi.