Imran Khan aonya juu ya njama za India dhidi ya Pakistan
Waziri Mkuu wa Pakistan ameonya juu ya njama chafu za India dhidi ya nchi yake.
Imran Khan ameashiria juu ya siasa na hatua za ukandamizaji za serikali ya India dhidi ya eneo la Kashmir na kuongeza kuwa, katika kujaribu kupotosha fikra za walio wengi juu ya hali mbaya ya eneo la Kashmir, New Delhi inaibua tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Pakistan. Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kwamba, huenda serikali ya India imeratibu operesheni za kigaidi kwa lengo la kujaribu kuonyesha kwamba operesheni hizo zimepangwa na Pakistan. Imran Khan ameashiria kwamba, India ilifutilia mbali haki ya mamlaka ya ndani ya eneo la Kashmir kwa madhara ya watu wa eneo hilo na baada ya hapo ikatekeleza utawala wa kijeshi kwenye eneo hilo jambo ambalo limewasababishia wakazi wake matatizo mengi.
Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa hatua ya serikali ya New Delhi ya kuweka vizuizi vingi na kuvuruga mawasiliano ya intaneti ya eneo la Kashmir inakusudia kuzuia habari za eneo hilo kufika nje. Ni miaka kadhaa sasa ambapo India imeweka maelfu ya askari katika maeneo ya Kashmiri yaliyo chini ya udhibiti wa serikali ya New Delhi. Katika uwanja huo, makumi ya maelfu ya watu wa eneo hilo wameuawa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Wakazi wa Kashmir wanataka kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufanyika kura ya maoni katika eneo hilo, suala ambalo linapingwa vikali na serikali ya India.