Katibu Mkuu wa NATO akiri: Mlingano wa nguvu duniani umebadilika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61559-katibu_mkuu_wa_nato_akiri_mlingano_wa_nguvu_duniani_umebadilika
Marekani ambayo ni kinara wa nchi za Magharibi imekuwa ikipinga suala la kuongezeka nguvu, ustawi na satua ya China katika uwanja wa kimataifa na imeitambua nchi hiyo kuwa ni tishio kwa ulimwengu wa Magharibi ikizitaka nchi za Ulaya kupunguza uhusiano wao na Beijing.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2020 03:32 UTC
  • Katibu Mkuu wa NATO akiri: Mlingano wa nguvu duniani umebadilika

Marekani ambayo ni kinara wa nchi za Magharibi imekuwa ikipinga suala la kuongezeka nguvu, ustawi na satua ya China katika uwanja wa kimataifa na imeitambua nchi hiyo kuwa ni tishio kwa ulimwengu wa Magharibi ikizitaka nchi za Ulaya kupunguza uhusiano wao na Beijing.

Hata hivyo msimamo huo wa Washington umekabiliwa na upinzani wa Umoja wa Ulaya, japokuwa Katibu Mkuu wa NATO ameonekana kuimba wimbo uleule wa Marekani. Jens Stoltenberg ameashiria ustawi na maendeleo ya China katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kijeshi na kiuchumi na kutoa wito wa kuwepo umoja zaidi baina ya nchi wanachama wa NATO kwa ajili ya kukabiliana na Beijing. Akizungumzia maendeleo makubwa ya China katika masuala ya kiuchumi na kijeshi amekiri kwamba, dunia inashuhudia mabadiliko ya mlingano wa nguvu. Jens Stoltenberg amesisitiza kwamba, nchi za Magharibi hazipaswi kupuuza ustawi mkubwa wa nguvu za China katika masuala ya kiuchumi na kijeshi. 

Katibu Mkuu wa NATO pia ameashiria athari mbaya za kiusalama zinazotokana na ustawi mkubwa wa China kwa washirika wa NATO na kusema: "Kwa sasa China inashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na bajeti kubwa zaidi ya masuala ya ulinzi na imewekeza sana katika masuala ya kisasa ya kijeshi; vilevile inamiliki makombora yanayoweza kulenga shabaha katika nchi wanachama wa NATO." 

Jens Stoltenberg

Inaonekana kuwa, shirika la NATO ambalo kivitendo limekuwa fimbo ya Washington ambayo inatumiwa kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Marekani hata dhidi ya waitifaki wake wa Ulaya, limeingia katika mzingo wa serikali ya Washington na sasa linazitaka nchi zote za Magharibi zikabiliane na China kwa shabaha ya kudhoofisha uwezo na nguvu yake inayostawi siku baada ya nyingine. Hata hivyo wito huo wa Katibu Mkuu wa NATO na serikali ya Donald Trump haujakaribishwa na nchi za Ulaya. Kimsingi tunaweza kusema kuwa, miongoni mwa hitilafu za waziwazi kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantic (Marekani na nchi za Ulaya) ni mitazamo inayotofautiana kikamilifu kuhusiana na China na uhusiano wao na nguvu hiyo inayostawi kwa kasi kiuchumi. Joseph Borell, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa: "China si tishio kwa usalama wa kimataifa na kuna ulazima wa kuwa na mwenendo unaotilia maanani ukweli wa mambo. Yumkini China ikawa mshindani wa Umoja wa Ulaya lakini sio tishio kwa uslama wa kimataifa.”

Joseph Borell

Yapata wiki mbili zilizopita pia Joseph Borell alisema kuwa, ushahidi unaonyesha kuwa, China inachukua nafasi ya Marekani kama kinara wa dunia nzima. Alisisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unashirikiana na Beijing katika masuala mengi ikiwa ni pamoja na katika kadhia ya kutetea na kulinda makubliano ya nyuklia ya JCPOA na Iran.

Tofauti na msimamo huo, maafisa wa serikali ya Donald Trump wamekuwa wakiitaja China kuwa ni tishio la kiuchumi na kiusalama. Baada ya kushika hatamu, rais huyo wa Marekani alianza kutekeleza siasa kali dhidi ya China na kuishinikiza Beijing kutokea pande zote. Hitilafu baina ya Marekani na China zinajumuisha nyanja mbalimbali za kisiasa, kibiashara, kiuchumi, masula ya usalama na ya kijeshi na hata katika masula ya kistratijia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo Jumatano ya juzi alitoa taarifa akiituhumu China kuwa inatumia mbinu za mabavu.

Mkabala wake, China pamoja na Russia ni miongoni mwa wapinzani wakuu wa siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Donald Trump kuhusiana na masula ya kimataifa na zinakosoa vikali sera za kiuchumi za kiongozi huyo. China pia inakosoa sana uchochezi wa kijeshi za Marekani baharini na angani na vilevile hatua za baadhi ya waitifaki wa serikali ya Washington kama Australia na Uingereza katika Bahari ya China Kusini.

Wang Yi 

Yote haya pamoja na sera za Washington za kuingilia mambo ya ndani ya China ikiwa ni pamoja na kuwachochea waandamanaji huko Hong Kong, vimezidisha ufa baina ya Beijing na Washington. Ni kwa sababu hii ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Nje wa China akasema kuwa, nchi hizi mbili zinakaribia kuingia katika vita baridi mpya.