UN yataka kufanyika marekebisho ya haraka katika muundo wa polisi Marekani
Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi jana Ijumaa iliitaka serikali ya Marekani kutetekeleza marekebisho haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuondoa ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika muundo wa polisi ya nchi hiyo.
Kamati hiyo imetoa taarifa na kuitaka serikali ya Marekani, viongozi wa serikali na maafisa wa nchi hiyo kutekeleza marekebisho ya haraka na yanayofaa kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ubaguzi wa kitaifa na ubaguzi wa rangi vinavyoshuhudiwa katika muundo wa polisi na idara za mahakama za nchi hiyo kwa kuzingatia haki za wahanga wa jinai zenye malengo ya utaifa.
Awali Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliutaja ubaguzi wa rangi nchini Marekani kuwa wa kimfumo na kulaani vitendo vya kibaguzi vinavyotekelezwa nchini humo. Bi Bachelet aidha alitahadharisha kuhusu mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa tena dhidi ya waandishi habari wanaoripoti juu ya maandamano kote nchini humo.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa sauti zinazotaka kuhitimishwa mauaji dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao hawana silaha zinapasa kusikika. Amesema pia sauti ambazo zinataka kukomeshwa ubaguzi wa rangi wa kimfumo ambao umeidhuru jamii ya Marekani zinapasa kusikika.
Ni zaidi ya wiki mbili sasa ambapo miji na majimbo mbalimbali ya Marekani yanashuhudia maandamano na ghasia kubwa za kulalamikia vitendo vya ubaguzi wa rangi vya polisi wa nchi hiyo kufuatia kuuliwa kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa jina la George Floyd. Katika kukabiliana na waandamanaji hao, polisi nchini Marekani inatumia mbinu mbalimbali zisizo za kiakhlaqi wala kibinadamu kwa kuwakanyaga na magari na kuwafyatulia risasi papo hapo.