China yasema mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran hayatafika popote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61791-china_yasema_mashinikizo_ya_marekani_dhidi_ya_iran_hayatafika_popote
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa amesema mashinikizo ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayatafika popote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2020 03:51 UTC
  • China yasema mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran hayatafika popote

Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa amesema mashinikizo ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayatafika popote.

Zhang Jun, Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa ametoa tamko hilo baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kusema vikwazo vya silaha dhidi ya Iran virefushwe ili Iran isiwezi kununua ndege za kivita kama vile SU-30 za Russia na J-10 za China.

Balozi Jun ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter na kusema, "Nafikiri mnafahamu ni nchi gani inauza silaha kwa wingi duniani."

Amesema azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liko wazi kuhusu Iran kuondolewa vikwazo vya silaha mwezi Oktoba.

Sambamba na kukaribia muda wa kufutwa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambavyo pia ni sehemu ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN, Wamarekani wanafanya njama kubwa kujaribu kuzuia kuhitimishwa vikwazo hivyo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hivi karibunii, serikali ya Marekani ilisambaza utangulizi wa azimio kwa wanachama wa baraza hilo ikiwataka warefushe muda wa vikwazo vya silaha vya umoja huo dhidi ya Iran. Pamoja na hayo upitishwaji wa azimio hilo unategemea kuungwa mkono na wanachama 9 wa Baraza la Usalama tena bila kupigiwa kura ya veto na China na Russia. 

Pamoja na kwamba Marekani kwa miaka miwili iliyopita na bila kuzingatia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama, ilijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, inadai katika tafsiri yake mpya kwamba kwa mujibu wa azimio hilo bado ni mmoja wa wanachama wenye taathira katika JCPOA.