Jul 03, 2020 00:39 UTC
  • Marekani na tuhuma mpya za kuwepo uhusiano kati ya Russia na Taliban

Mwaka 2001 Marekani iliishambulia kijeshi na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kutumia kisingizio cha mashambulio ya Septemba 11 yaliyolenga sehemu kadhaa ndani ya ardhi ya Marekani. Wakati rais wa Marekani Donald Trump alipokuwa katika kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2016 na hata baada ya kuingia ikulu ya White House aliahidi kuwa atawaondoa askari wa nchi hiyo walioko Afghanistan. Hata hivyo pamoja na ahadi hiyo, askari wengi wa jeshi la Marekani wangaliko katika ardhi ya Afghanistan.

Hivi sasa maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani wakiwemo wa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentagon wanaielekezea kidole cha tuhuma Russia kuwa inaingilia masuala ya Afghanistan na inashirikiana pia na Taliban ili kwa njia hiyo wapate kisingizio cha kutetea kushindwa kwa Washington na kupata sababu ya kuendelea kuwepo kijeshi nchini humo. Miongoni mwa viongozi wa Marekani walioituhumu Russia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Mike Pompeo ambaye amesema, Russia inapinga Marekani kuwepo Afghanistan na inaliuzia silaha kundi la Taliban. Akiongea na waandishi wa habari Pompeo amesema: "Ni ukweli kwamba Russia inafanya mambo yake Afghanistan ili kukabiliana na Marekani; na hili si jambo jipya. Kwa miaka 10 Warussia wanaiuzia Taliban silaha mbalimbali na jambo hili linahatarisha maisha ya Wamarekani. Tumelalamikia suala hili na kila nilipokutana na mwenzangu wa Russia nimekuwa nikimwambia: "Simamisheni jambo hili."

Rais Vladimir  Putin wa Russia (kulia) na wanamgambo wa Taliban

Hata hivyo Russia imekanusha mara kadhaa madai ya Marekani kwamba inawauzia silaha Taliban.

Katika msimamo mwengine ulioonyeshwa na Marekani, siku ya Jumatano wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentagon ilitoa ripoti ikidai kwamba, serikali ya Russia imeshirikiana na Taliban kwa ajili ya "kuharakisha kuondoka askari wa Marekani" nchini Afghanistan. Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la "Uimarishaji usalama na uthabiti Afghanistan", Pentagon imedai kuwa, Moscow inashirikiana na Taliban kuidhoofisha serikali ya Afghanistan. Katika ripoti hiyo ya Pentagon imedaiwa kuwa: "Russia inaisaidia kisiasa Taliban ili kuwa na ushawishi ndani ya kundi hilo, kufupisha muda wa kuwepo kijeshi askari wa Magharibi na kuimarisha operesheni dhidi ya DAESH (ISIS), ijapokuwa katika duru rasmi inakanusha kuwepo kwa mahusiano hayo." Baadhi ya wachambuzi wanasema, ripoti hiyo mpya ya Pentagon ina maana ya kutangaza rasmi madai ya kuwepo uhusiano kati ya Russia na Taliban.

Msimamo huo wa madai dhidi ya Russia umechukuliwa huku Kongresi ya Marekani na wabunge wa chama wa Democrat hususan Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi akitaka zichukuliwe hatua kali dhidi ya Moscow hasa za kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Bi Pelosi amechukua msimamo huo kufuatia ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na gazeti la New York Times iliyoeleza kwamba, idara ya intelijensia ya jeshi la Russia ijulikanayo kwa ufupi kama GRU ilifanya muamala na Taliban huko nyuma na kuwaahidi kuwa itawapatia bakhshishi ya fedha taslimu kwa kila askari mmoja wa Marekani watakayemuua huko Afghanistan. Kwa mujibu wa madai yaliyotolewa na gazeti hilo, maafisa wa intelijensia wa Marekani walimjulisha rais wa nchi hiyo Donald Trump kuhusu hatua hiyo ya Russia. Ripoti hiyo ya New York Times ilichapishwa tena baadaye na magazeti ya Washington Post na Wall Street Journal kwa kunukuu "duru za ndani ya White House".

Kutoka kulia juu: Trump, Putin na wanajeshi wa US Afghanistan. Chini kulia: Wanamgambo wa Taliban na askari wa Marekani wakibeba jeneza la askari mwenzao

Hata hivyo madai hayo yamekadhibishwa vikali na Taliban na Russia na hata Trump mwenyewe. Kwa mujibu wa rais huyo wa Marekani, yeye na washauri wake wa karibu hawajawahi kupatiwa taarifa zozote kuhusu ripoti inayohusiana na "mashambulio yanayodaiwa" kufanywa dhidi askari wa Marekani nchini Afghanistan kwa msaada na uungaji mkono wa Russia. Trump amekanusha ripoti ya gazeti la New York Times kuhusiana na suala hilo akiitaja kuwa ni habari "feki". Katika ujumbe alioandika siku ya Jumatatu kwenye akaunti yake ya Twitter, rais huyo wa Marekani aliandika: "Taasisi ya intelijensia ya Marekani imenipa ripoti kuwa haioni kama taarifa hizi ni za kuaminika na ndiyo maana hawakuziripoti kwanga au kwa makamu wangu." 

Aprili 29, 2020 serikali ya Trump ilisaini makubaliano na Taliban, ambayo moja ya vipengee vyake kinahusu kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan. Tangu mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa hakuna askari wa Marekani aliyeuliwa na Taliban na idadi ya askari wa nchi hiyo walioko Afghanistan imepungua kutoka 13,000 hadi 8,600.

Russia kwa upande wake inahisi kuwa lengo hasa la waliozusha madai hayo ni kuzidi kuuharibu uhusiano wa Moscow na Washington na vilevile kupata kisingizio kipya  cha kuzidishia mashinikizo ya Marekani dhidi ya Russia na wakati huohuo hiyo ni hatua inayochukuliwa na Wademocrat kwa madhumuni ya kuichafua zaidi haiba ya Trump katika kipindi hiki kilichosalia hadi utakapofanyika uchaguzu wa urais wa Marekani Novemba mwaka huu kwa kumuonyesha Trump kuwa ni kikaragosi cha Russia. Zamir Kabolov, mwakilishi maalumu wa rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan amesema: "Moscow inazichukulia ripoti za vyombo vya habari za madai kuhusu pendekezo la kuwapatia fedha Taliban kwa ajili ya kuwaua wanajeshi wa Marekani kuwa ni "ugomvi wa kisiasa wa ndani ya Marekani" kwa sababu mirengo inayopendelea nchi hiyo iwepo kijeshi Afghanistan inatumia habari feki ili kutetea kushindwa kwao nchini Afghanistan.../

Tags