Bolton: Ni baidi Trump kushinda tena katika uchaguzi wa urais 2020
Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani amesema, ni jambo lililo mbali kwa Donald Trump kushinda tena katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.
John Bolton, ambaye katika wiki za karibuni amefichua mambo kadhaa yaliyoharibu na kuichafua shakhsia ya Donald Trump, amekosoa mtazamo na muelekeo wa rais huyo wa Marekani na kueleza kwamba, uwezekano wa yeye Trump kuendelea kusalia katika Ikulu ya White House unazidi kupungua.
Bolton ameongeza kuwa: Yeye Trump si Mrepublican mhafidhina wala si Mdemocrat wa Kiliberali bali ni mtu mwenye falsafa yake binafsi anayofuata.
Mshauri huyo wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani katika serikali ya Trump mwenyewe, ambaye uhusiano wake na kiongozi huyo umeharibika sana, amesema kuhusu uchaguzi ujao wa rais wa nchi hiyo kwamba: Kwa mara ya kwanza nimeshaamua kutompigia kura mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi.
Kulingana na kauli ya Bolton, Trump bado hajaweza kuelewa sawasawa, kuwa rais kuna uzito na umuhimu gani.
Ikiwa imesalia miezi minne tu kabla ya kufanyika uchaguzi wa urais wa Marekani, hivi sasa Trump ametingwa na matatizo chungu nzima ya kiuongozi. Kutoridhishwa Wamarekani na jinsi Trump anavyoiongoza nchi kunashuhudiwa pia hata miongoni mwa waungaji mkono wake wa zamani ndani ya chama chake cha Republican.
Wakati huohuo chunguzi mbali mbali za maoni zinazoendelea kufanywa nchini Marekani zinaonyesha kuwa, kukubalika kwa Trump mbele ya wananchi kunazidi kupungua na endapo uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utafanyika hivi sasa, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrat Joe Biden atamshinda vibaya Trump katika kinyang'anyiro hicho.../