Trump aendelea kumdhihaki Biden, sasa ataka apimwe madawa ya kulevya
Rais wa Marekani ameendelea kumkejeli mshindani wake mkuu wa chama cha Democrat katika uchaguzi ujao wa rais kwa kutaka afanyiwe vipimo vya madawa ya kulevya kabla ya kufanyika midahalo baina yao ya kampeni za uchaguzi.
Donald Trump ametoa kauli hiyo ya istihzai dhidi ya Joe Biden katika mahojiano maalumu na gazeti la Washington Examiner na kudai kwamba, katika midahalo ya ndani ya chama chake cha Democrat, Joe Biden alifanya vibaya sana lakini ghafla akang'ara mno katika midahalo ya mwishoni.
Trump amesisitiza kuwa, kutokana na kupiga hatua ghafla Biden kiuwezo katika kufanya mdahalo, anataka mgombea huyo wa chama cha Democrat afanyiwe vipimo vya mihadarati kabla ya kuanza midahalo baina yao ya kampeni za uchaguzi wa urais.
Mdahalo wa kwanza kati ya Trump na Biden umepangwa kufanyika mwezi ujao wa Septemba.
Trump ameshatoa kauli mara kadhaa za kumkejeli na kumfanyia istihzai Joe Biden kwa sababu ya tatizo alilonalo la ulimi mzito, linalomfanya baadhi ya wakati atamke maneno kimakosa.
Uchaguzi wa urais wa Marekani utafanyika tarehe 3 ya mwezi Novemba.../