Congress: Trump ndiye sababu ya kuongezeka machafuko nchini Marekani
Mkuu wa Kamati ya Kutoa Taarifa ya Baraza la Congress la Marekani amemlaumu vikali rais wa nchi hiyo Donald Trump na kusema kuwa, vitendo vya kichochezi vya rais huyo ndiyo sababu ya kuzuka na kuongezeka machafuko nchini Marekani.
Adam Schiff amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya CNN ya Marekani na kuongeza kuwa, Trump anadhani kwamba kutumia nguvu na mabavu na kuwakandamiza wananchi wanaoandamana kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo kutamsaidia katika uchaguzi ujao. Amesema huo ndio ukweli wa kuhuzunisha, wa kutisha na wa kutia majonzi kuhusu rais huyo wa Marekani.
Mkuu huyo wa Kamati ya Kutoa Taarifa ya Baraza la Congress la Marekani ameongeza kuwa, Trump anawasha kwa makusudi moto wa machafuko nchini humo.
Itakumbukwa kuwa, afisa mmoja mzungu wa polisi, tarehe 25 Mei mwaka huu alimuua kikatili na kwa damu baridi kabisa George Floyd, raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis wa jimbo la Minnesota la magharibi mwa Marekani.
Jinai hiyo ya afisa mzungu wa polisi wa Marekani mwenye chuki na watu wa rangi nyingine hasa Wamarekani wenye asili ya Afrika, imezusha fujo na maandamano makubwa ya Marekani nzima.
Hata hivyo, badala ya kutoa maneno ya kutuliza hasira za waandamanaji, Trump aliwatukana waandamanaji hao akiwaita ni majambazi na waporaji. Aidha alitoa amri kwa polisi na askari usalama wa Marekani kutumia nguvu kuwakandamiza waandamanaji hao.
Hata hivyo maandamano bado yanaendelea ambapo katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya wananchi wa Marekani wamejeruhiwa na kutiwa nguvuni katika maandamano hayo.