Sanders: Wamarekani milioni 10 wanasumbuliwa na njaa na ukosefu wa ajira
Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani amefichua kuwa, raia milioni 10 wa nchi hiyo wanasumbuliwa na njaa na ukosefu wa ajira.
Bernie Sanders alisema hayo jana Jumatatu katika ujumbe aliotuma kwenye mtandano wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, janga la corona limeshadidisha matatizo ya Wamarekani.
Mwanasiasa huyo ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Donald Trump amebainisha kuwa: Mdororo wa uchumi nchini (Marekani) umewaweka Wamarekani milioni 10 katika hatari ya kufa njaa na kupoteza ajira.
Sanders amekuwa akikosoa utendaji kazi wa Trump hususan katika kukabiliana na janga la virusi vya corona.
Badala ya kuandaa na sera na mikakati ya kupambana na janga hilo, Trump amekuwa akizilaumu China na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mripuko huo. Utepetevu huo wa Trump umepelekea kuporomoka kwa kiasi kikubwa uungaji mkono wa Wamarekani kwake.
Marekani inasalia kuwa nchi yenye maambukizi na vifo vingi zaidi vya ugonjwa wa Covid-19 duniani, licha ya kuwa ni taifa lenye uchumi mkubwa zaidi.