Ilhan Omar: Trump ni dikteta na mbaguzi wa rangi
Ilhan Omar, Mbunge mwanamke Muislamu katika Kongresi ya Marekani amesema, rais wa nchi hiyo Donald Trump ni mtu dikteta na mbaguzi wa rangi.
Ilhan Omar ameliambia gazeti la The Independent linalochapishwa Uingereza: "Rais wa nchi hii Donald Trump ni mtu dikteta na mbaguzi wa rangi, lakini Marekani inaweza kukivuka kipindi chake cha urais na Trump atashindwa katika uchaguzi."
Kwa mujibu wa Ilhan Omar, ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Minnesota katika Baraza la Wawakilishi la Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat, Trump ameitumia vibaya imani ya wananchi kwake.
Ilhan Omar amesisitiza kuwa: Malengo ya Wademocrat baada ya mgombea wao Joe Biden kushinda katika uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba 3, ni kutekeleza mpango wa huduma za matibabu bila malipo, kuwakomboa Wamarekani wanachuo milioni 45 wenye madeni ya masomo, kuhitimisha janga la tabianchi na kujikita katika kutekeleza sera za kiutu kuhusiana na uhajiri.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa Biden amemtangulia Trump kwa kuungwa mkono na wapigakura wengi zaidi.
Utendaji mbovu wa Trump katika kulikabili janga la dunia nzima la virusi vya corona na msimamo wake wa kuunga mkono ukandamizaji dhidi ya maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani vimeibua upinzani mkubwa na malalamiko ya wananchi wengi wa nchi hiyo.../