Trump ni tishio kwa usalama wa Marekani
Mkuu wa Kamisheni ya Habari katika Congress ya Marekani amesema Rais Donald Trump ni hatari na tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo.
Akizungumza karibuni na televisheni ya CNN kuhusu hatua ya Rais Trump ya kukwepa kulipa kodi, Adam Schiff amesema kuwa Trump anadaiwa dola milioni 400 na kwamba jambo hilo linahesabiwa kuwa tatizo kubwa katika kitengo cha usalama wa taifa.
Katika mdahalo wao wa kwanza wa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika hapo tarehe 3 mwezi ujao wa Novemba, Joe Biden, mgombea wa chama cha Democrat aliashiria suala la Trump kukataa kuchapisha nyaraka zake za ulipaji kodi.
Kabla ya hapo gazeti la New York Times lilitegemea nyaraka hizo za kodi na kuandika kwamba mwaka 2016 Trump alilipa kodi ya dola 750 tu.
Rais huyo wa Marekani alikanusha na kulalamikia vikali ripoti hiyo ya New York Times kuhusiana na suala la kukwepa kwake kulipa kodi.
Kukataa kulipa kodi nchini Marekani ni kashfa kubwa ambayo imepelekea viongozi wengi wa kisiasa wa nchi hiyo kujiuzulu.