NBC News: Trump sasa anatafunwa na istihzai zake kuhusu COVID-19
Kanali ya televisheni ya NBC News ya nchini Marekani imesema kuwa, rais wa nchi hiyo, familia na wafuasi wake sasa wanatafunwa na matamshi ya istihzai na hatua zisizo sahihi za Donald Trump kuhusu ugonjwa wa COVID-19.
Televisheni hiyo imemlaumu vikali Donald Trump (74), kwa kuitisha mkutano mkubwa ambao baadhi ya washiriki wake walikaa ndani ya eneo lililozibwa kila mahali bila ya kuvaa barakoa huku Trump akijigamba kuwa corona itaisha karibu tu, wakati ambapo kitendo chake hicho kimehatarisha usalama wake mwenyewe na wa wafanyakazi wake.
Kanali hiyo ya televisheni ya Marekani imeongeza kuwa: "Trump amekuwa muhanga wa jumbe zake ghalati kuhusu corona."
Itakumbukwa kuwa, rais huyo wa Marekani muda wote amekuwa akiufanyia istihzai ugonjwa wa COVID-19 kiasi kwamba kuna wakati alishauri wagonjwa wa corona wadungwe na wanyweshwe vitakasaji (sanitizers) ndipo wataweza kupona.
Alkhamisi usiku, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba yeye na mkewe wamekumbwa na ugonjwa wa COVID-19.
Saa moja baadaye Trump alitangaza kwamba hata Hope Hicks, mmoja wa washauri wake wa karibu naye amekumbwa na corona.
Daktari Sanjay Gupta, mwandishi mwandamizi wa masuala ya tiba wa televisheni ya CNN anasema, serikali ya Trump sasa inapaswa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu watu walionana na wagonjwa hao wapya wa COVID-19 na kuchukuliwe hatua za lazima za kuwekwa chini ya karantini.
Hadi Ijumaa usiku, Wamarekani wasiopungua 212,883 walishafariki dunia na zaidi ya 7,505,749 walishambukizwa kirusi cha corona nchini humo.
Serikali ya Marekani na hasa rais Donald Trump mwenyewe amelaumiwa na kukosolewa vikali kwa kutowajibika ipasavyo katika kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona katika nchi hiyo