Trump asema hatashiriki mdahalo wa urais kwa njia ya mtandao
Rais Donald Trump amesema hatoshiriki mdahalo wa pili wa wagombea wa urais nchini Marekani iwapo utafanyika kwa njia ya intaneti.
Trump alisema hayo jana Alkhamisi muda mfupi baada ya Kamisheni ya Midahao ya Urais nchini humo kusema mdahalo wa pili baina ya Trump wa chama tawala cha Republican na Joe Biden wa chama cha upinzani cha Democrat utafanyika kwa njia ya intaneti kutokana na Trump kuambukizwa virusi vya corona.
Bill Stepien, Mkurugenzi wa Kampeni za Trump ameikosoa kamisheni hiyo akidai kuwa imempendelea Joe Biden. Bideni alisema hivi karibuni kuwa hayuko tayari kushiriki mdahalo wa ana kwa ana na Trump hadi pale rais huyo wa Marekani atakapopimwa na kuthibiti kuwa hana tena ugonjwa wa Covid-19.
Kamisheni ya Midahalo ya Urais nchini Marekani imesema imechukua uamuzi wa kubadili mtindo wa mdahalo huo unaotazamiwa kufanyika Oktoba 15 huko Florida, ili kulinda usalama na afya ya wahusika wote. Mdahalo huo ulitazamiwa kuwa na hadhira ambao wangewauliza maswali wagombea hao wa urais moja kwa moja.
Itakumbukwa kuwa, asilimia 69 ya Wamarekani walisema wamechukizwa na mdahalo wa kwanza uliofanyika Septemba 29, na kusisitiza kwamba haukuwa na thamani na uliibua wasi wasi kuhusu mustakabali wa Marekani.
Mdahalo huo ambao ulifanyika katika Chuo Kikuu cha Case Western Reserve Cleveland, Ohio uligeuka na kuwa jukwaa la shutuma, tuhuma na kufokeana.