Pompeo ahalalisha mauzo ya silaha kwa Saudia kwa kuichafua Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amekariri tuhuma na madai yake yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kutumia uenezaji huo wa chuki dhidi ya Iran kuhalalisha mauzo ya silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola za US kwa Saudi Arabia.
Mike Pompeo alikutana na Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia mjini Washington jana Jumatano na kudai kuwa, Marekani itaendelea kuiuzia silaha Riyadh ili ijihami, na eti Iran inahatarisha usalama wa Saudia na eneo zima la Asia Magharibi, kwa kuiunga mkono harakati ya Houthi (Ansarullah) ya Yemen.
Pompeo amekariri porojo zake kwa kudai kuwa makombora ya balestiki yanayotumiwa na wapiganaji wa Houthi wa Yemen kupiga vituo vya mafuta vya Saudia ni ya Iran na kwamba ndege zisizo na rubani za Ansarullah zimetengezwa kwa kutumia teknolojia ya Tehran.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa, Marekani ndio muuzaji mkubwa zaidi wa silaha duniani huku Saudi Arabia ikishika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Asia Magharibi. Saudia inatumia silaha hizo kuwaua wananchi wa Yemen na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo maskini jirani yake.
Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameashiria kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain na kueleza bayana kuwa, anataraji Saudia itafuata mkumbo huo.
Mike Pompeo amedai kuwa, mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya Iran yamefanikiwa kukata kikamilifu mishipa ya kufikiwa na fedha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.