Wafuasi wa Trump wenye bunduki wazingira vituo vya kuhesabu kura
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64479-wafuasi_wa_trump_wenye_bunduki_wazingira_vituo_vya_kuhesabu_kura
Idadi kubwa ya wafuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani wameonekana katika vituo kadhaa vya kuhesabu kura nchini humo wakiwa wamebeba bunduki za rashasha.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Nov 07, 2020 04:09 UTC
  • Wafuasi wa Trump wenye bunduki wazingira vituo vya kuhesabu kura

Idadi kubwa ya wafuasi wa Rais Donald Trump wa Marekani wameonekana katika vituo kadhaa vya kuhesabu kura nchini humo wakiwa wamebeba bunduki za rashasha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Associated Press, wafuasi hao wa Trump ambao wanaandamana wakilalamikia matokeo ya uchaguzi ni wachache lakini wameibua hofu kutokana na silaha walizobeba wakiwa wamevalia sare za kijeshi.

Kati ya maeneo ambayo wanamgambo hao wa Trump wameonekana ni katika majimbo ya Arizona, Nevada na Michigan. Majimbo hayo huwaruhusu watu kubeba silaha hadharani. Wafuasi hao wa Trump waliojizatiti kwa silaha wanaunga mkono madai ya mtawala huyo wa Marekani kuwa kuna wizi wa kura katika uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba tatu. Maafisa wanaohesabu kura katika majimbo ambayo mgombea wa chama cha upinzani cha Democratic Joe Biden anaongoza wamesema wanahofia maisha yao.

Joe Biden (kushoto) na Donald Trump

Akizungumza mapema leo,  Biden ameashiria kuhusu uwezekano kuwa atapata ushindi huku akitoa wito kwa Wamarekani kuwa watulivu.

Hadi sasa Biden, mwenye umri wa miaka 77 ana kura 264 wakati Trump ana kura 214 katika jopo linalomchagua rais la Electoral College lenye wanachama 538 ambapo mshindi anahitajika kupata kwa uchache kura 270 ili kutangazwa mshindi. Aidha Biden hadi sasa amepata asilimia 50.6 ya jumla ya kura zote zilizopigwa na wananchi huku Trump akiwa na asilimia 47.7 ya kura. Katika uchaguzi wa Marekani mshindi hapatikani kwa wingi wa kura za wananchi bali ni kura zinazopigwa na wanachama hao wachache wa jopo la Electoral Collage.

Akizungumza leo katika Ikulu, Rais Trump amewashambulia wapinzani wake, akidai wanalenga kufanya udanganyifu dhidi yake.