Dec 21, 2020 13:45 UTC
  • Kuanza kuondoka askari wa jeshi la Marekani nchini Somalia; kujipanga upya kijeshi Washington barani Afrika

Marekani imeanza kuwaondoa wanajeshi wake walioko nchini Somalia kwa madhumuni ya kuwapeleka katika vituo vyake vingine mashariki mwa Afrika.

Kwa mujibu wa msemaji wa Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM, siku ya Jumamosi, manowari ya nchi hiyo ya USS Africa Hershel Woody Williams, ilianza kutekeleza "operesheni ya baharini katika pwani ya Somalia". Lengo la kutekelezwa operesheni hiyo ni kuwaondoa wanajeshi wa Marekani nchini Somalia na kuwapeleka katika nchi zingine za Afrika.

Askari wa Marekani walioko Somalia kwa kile kilichotajwa kutoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo

Jeshi la Marekani liliwapeleka askari wake mia saba nchini Somalia kwa kisingizio cha kupambana na kundi lenye misimamo ya kufurutu ada la Ash-Shabaab. Ilivyodai wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon, wanajeshi hao waliopelekwa Somalia walikuwa wakitoa mafunzo kwa askari wa nchi hiyo ya kukabiliana na makundi ya Al Qaeda na Ash-Shabaab. Donald Trump, ambaye hivi sasa anakamilisha siku zake za mwisho katika ikulu ya White House, mnamo mwanzoni wa mwezi huu wa Desemba alichukua uamuzi muhimu wa kijeshi, wa kuamuru wanajeshi wa Marekani walioko Somalia wawe wameshaondoka katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita ifikapo mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2021. Marekani ina jumla ya askari wapatao elfu sita katika kila pembe ya bara la Afrika na vituo vipatavyo 29 vya kijeshi katika nchi za bara hilo.

Inavyoonekana, kuna sababu na malengo tofauti ya nyuma ya pazia la uamuzi huo uliochukuliwa na serikali ya Trump. Kwanza ni kwamba Trump anajaribu kuwaaminisha Wamarekani kwamba, ameheshimu na kutekeleza ahadi alizotoa katika kampeni zake za uchaguzi wa rais hadi siku za mwisho za uongozi wake; na kwa kufanya hivyo, kujiongezea fursa ya ushindi katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2024.

Donald Trump

Suala jengine ni kwamba, Donald Trump amekuwa na mtazamo na muelekeo tofauti na wa marais waliomtangulia, kuhusiana na kuwepo vikosi vya jeshi la Marekani nje ya nchi hiyo, ambao ni wa kuzingatia faida za kiuchumi badala ya maslahi matupu. Kwa mtazamo wa Trump, kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani nje ya nchi hiyo, ambako kuna gharama kubwa kifedha, lazima kuendane na mantiki ya manufaa na faida za kiuchumi. Kwa maneno mengine ni kwamba, anachotaka yeye, gharama za kuwaweka wanajeshi hao zilipwe na nchi zinazowapokea, na wakati huohuo kuwepo kwao katika nchi hizo kuinufaishe kifedha pia Washington. Kwa ajili ya kufikia lengo hilo, Trump ametoa mashinikizo makubwa kwa waitifaki wa kikanda wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan magharibi na mashariki ya Asia ya kuwataka waongeze michango yao ya kugharimia askari wa jeshi la nchi hiyo. Lakini kwa upande wa askari wa Marekani waliopelekwa barani Afrika, kwa kuzingatia hali ya umasikini ya nchi kama Somalia, isingeyumkinika kwa Washington kuibua takwa kama hilo. Kwa hiyo ili kupunguza gharama za kuwepo kijeshi Washington barani Afrika, serikali ya Trump imeamua kuziunganisha pamoja kamandi zake za kijeshi za Ulaya na Afrika. Uamuzi huo ni hatua ya kwanza kuchukuliwa katika wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ili kuangalia upya na kwa mapana kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika kila pembe ya dunia, lengo likiwa ni kufanya juhudi za kupanga mkakati bora zaidi wa uwepo kijeshi wa Washington, kwa kuainisha vipaumbele vyake vya kiulinzi, huku China na Russia zikitajwa kuwa ndio tishio kuu kwa Marekani.

Kuhusiana na hayo, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, kamandi ya vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Marekani ilieleza katika taarifa kwamba, Kamandi ya Kijeshi ya Marekani barani Ulaya EUCOM na ile ya Afrika AFRICOM zinaunganishwa pamoja kwa madhumuni ya kuongeza uwezo wa kufanikisha malengo ya kistratejia na ya operesheni za nchi hiyo Ulaya na Afrika. Tangu mwezi Februari mwaka huu wa 2020 Pentagon ilikuwa imeshatangaza dhamira yake ya kuratibu na kupanga upya uwepo kijeshi wa Marekani barani Afrika.

Kuhusiana na suala hilo, kamanda wa zamani wa AFRICOM Jenerali Roger Cloutier anasema: "Ujumbe wangu kwa washirika wetu wa Afrika ni kwamba hatutakuacheni mkono, bali tutaendelea kufanya kazi pamoja na nyinyi."

Lakini licha ya kutolewa ahadi hiyo, ukweli ni kwamba hivi sasa Marekani iko taabani ikiwa na upungufu mkubwa wa fedha; na kwa hivyo haiwezi kuhimili gharama kubwa za kuendelea kuwaweka askari hao. Kwa hivyo inatumia visingizio mbalimbali ili kujaribu kupunguza na kuvichanganya pamoja vikosi vya jeshi lake vilivyoko nje ya nchi, jambo ambalo utekelezaji wake uko mashakani kwa kutilia maanani upinzani wa mirengo ya ndani ya nchi hiyo inayoshabikia sera za utumizi wa nguvu za kijeshi katika siasa za Marekani.../ 

Tags