UN: Wanasiasa Marekani waheshimu mchakato wa kidemokrasia na utawala wa sheria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65635-un_wanasiasa_marekani_waheshimu_mchakato_wa_kidemokrasia_na_utawala_wa_sheria
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na yaliyojiri Jumatano mjini Washington DC nchini Marekani na kuwataka viongozi wa kisiasa kuwaasa wafuasi wao kujizuia na ghasia.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 07, 2021 06:13 UTC
  • Wafuasi wa Trump wakiwa ndani ya jengo la Bunge la Congress
    Wafuasi wa Trump wakiwa ndani ya jengo la Bunge la Congress

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na yaliyojiri Jumatano mjini Washington DC nchini Marekani na kuwataka viongozi wa kisiasa kuwaasa wafuasi wao kujizuia na ghasia.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa UN Stephane Dujarric akijibu swali kwenye mkutano na waandishi wa Habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa alipoulizwa kuhusu kauli ya Umoja wa Mataifa kufuatia mamia ya waandamanaji kuvamia jengo kuu la serikali na bunge la Congress amesema “Katibu Mkuu ameshtushwa sana na matukio kwenye mji mkuu wa Marekani Washington DC Jumatano. Na katika mazingira hayo ni muhimu kwamba viongozi wa kisiasa kuwasisitiza wafuasi wao haja ya kujizuia na machafuko ,lakini pia kuheshimu mchakato wa kidemokrasia na utawala wa sheria.”

Mfuasi wa Trump akiwa amekalia kitu katika Bunge la Congress baada ya kuvamia eneo hilo

Maelfu ya wafuasi wa rais wa chama tawala wameandama kuvamia jengo kuu mjini Washington DC kwenye bunge la Congress ambako wabunge walikuwa wanakutana kuhesabu kura za wawakilishi wa majimbo 50 ambao kimsingi ndio wanaoamua nani awe  rais. Wafuasi wa Trump walivamia kikao hicho na kuteka bunge kwa masaa kadhaa na hivyo kupelekea kikao kusitishwa kwa muda. Watu wasiopungua wanne wameuawa katika ghasia hizo. Kuna wasiwasi mkubwa kuwa  baada ya Bunge la Congress kumuidhinisha Biden kuwa rais wa Marekani, wafuasi wa Trump watendeleza maandamano na ghasia kote katika nchi hiyo ambayo sasa imegawanyika katika kambi mbili hasimu.