Akthari ya Wamarekani wanataka Trump aondolewe madarakani haraka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i65674-akthari_ya_wamarekani_wanataka_trump_aondolewe_madarakani_haraka
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani yanaonyesha kuwa, baada ya jengo la Kongresi kushambuliwa na kuvamiwa na wafuasi wa Rais Donald Trump, Wamarekani wengi wanataka kiongozi huyo aondolewe madarakani haraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2021 09:24 UTC
  • Akthari ya Wamarekani wanataka Trump aondolewe madarakani haraka

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani yanaonyesha kuwa, baada ya jengo la Kongresi kushambuliwa na kuvamiwa na wafuasi wa Rais Donald Trump, Wamarekani wengi wanataka kiongozi huyo aondolewe madarakani haraka.

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Reuters na taasisi ya Ipsos yanaonyesha kuwa asilimia 57 ya Wamarekani wanaitakidi kuwa, Trump anapasa auzuliwe mara moja wadhifa wa urais kwa sababu ya kuwachochea wafuasi wake wavamie jengo la Kongresi.

Akthari ya Wademocrat walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni wamesema, rais Donald Trump inatakiwa aondolewe madarakani sasa hivi kwa sababu ya kuanzisha uasi ndani ya Marekani.

Hata hivyo Warepublican wana mtazamo tofauti na huo na wanataka kiongozi huyo aendelee kubakia madarakani hadi kipindi chake cha urais kitakapomalizika kisheria.

Matokeo hayo ya uchunguzi huo wa maoni aidha yanaonyesha kuwa, kati ya kila Wamarekani 10 waliompigia kura Trump katika uchaguzi wa rais, saba miongoni mwao wamelaani shambulio lililofanywa na wafuasi wake dhidi ya jengo la bunge la nchi hiyo.

Wafuasi wa Trump baada ya kuvamia jengo la Kongresi

Sambamba na kufanyika kikao cha pamoja cha Kongresi ya Marekani, kilichojumuisha Maseneta na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kwa lengo la kuidhinisha rasmi ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba 3, wafuasi kadhaa wa Trump waliokuwa wamekusanyika mbele ya jengo la bunge walivamia jengo hilo na kukwamisha mchakato huo kwa saa kadhaa.

Watu watano waliuawa katika mtafaruku na machafuko yaliyozuka kufuatia uvamizi huo.

Hadi sasa viongozi na maafisa wengi wa zamani na wa sasa wa serikali ya Marekani wamelaani hujuma na uvamizi uliofanywa na wafuasi wa Donald Trump katika jengo la Kongresi ya nchi hiyo.../