Pence abariki mchakato wa kuuzuliwa Trump
Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema kuwa kuna uwezekana kutumia kifungu cha 25 cha Katiba kwa ajili ya kumuuzulu Rais Donald Trump.
Televisheni ya CNN imeripoti kuwa, Mike Pence amesema yumkini kutumia kifungu hicho kumuuzulu Donald Trump na kuongeza kuwa: Iwapo rais Trump ataendeleza chokochoko zake kuna uwezekano wa kuchukuliwa hatua hiyo.
Wakati huo huo duru za kuaminika zimetangaza kuwa, Mike Pence amesema atashiriki katika sherehe ya kuapishwa rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden itakayofanyika tarehe 20 mwezi huu. Hii ni licha ya Trump kutangaza kuwa hatashiriki katika sherehe hiyo ya kupokezana madaraka na kuapishwa Biden.
Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameutaja uamuzi huo wa Donald Trump kuwa ni aibu kwa dunia.
Jumatano iliyopita wafuasi wa Donald Trump walishambulia jengo la Kongresi ya Marekani na kuliteka kwa masaa kadhaa. Watu wasiopungua 5 waliuawa katika shambulizi na uvamizi huo. Biden amelitaja tukio hilo kuwa ni siku nyeusi zaidi katika historia ya Marekani.