Polisi ya Ufaransa imemtahadharisha Macron kuhusu kuongezeka ghasia za mitaani
Polisi ya ufaransa imemtahadharisha Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo kuhusu kuongezeka ghasia na machafuko ya mitaani.
Afisa mmoja wa polisi katika mji wa Montpellier amemweleza Rais Emmanuel Macron wakati alipoyatembelea maeneo yaliyoathiriwa pakubwa na machafuko katika mji huo kwamba: Sisi tunakabiliana na vijana waliojizatiti pakubwa huku wakiwa na silaha nyingi.
Polisi mwingine amemweleza Rais Macron kwamba vitendo vya ghasia na utumiaji mabavu vimekuwa ni jambo la kawaida katika maandamano dhidi ya serikali kwa jina la maandamano ya harakati ya vizibao vya njano.
Rais Macron amesema kuwa serikali itaongeza askari usalama na polisi elfu kumi hadi kumalizika muhula wake wa urais wa miaka mitano nchini Ufaransa. Amesema kuwa, hatua hiyo ni katika jitihada za kuboresha hali ya usalama na kupunguza jinai nchini humo.
Rais wa Ufaransa amesema kuna ulazima wa kuasisiwa shule ya kijeshi au kutolewa mafunzo endelevu kwa askari polisi katika mji wa Montpellier na kwamba kuna udharura pia wa kubadilishwa sare zao. Amesema katika akademia hiyo ya kijeshi askari polisi watapata mafunzo kwa muda wa miezi mitatu hadi sita. Rais Macron ameyaeleza hayo wakati ambapo wananchi wa Ufaransa wamelalamika na kupinga mara kadhaa vitendo vya utumiaji mabavu vinavyofanywa na polisi wa nchi hiyo na hatua kali za udhibiti za serikali ya nchi hiyo kuhusu udumishaji amani, utelekezaji sheria na kuwakingia kifua polisi.