May 29, 2021 03:02 UTC
  • Ripoti ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN kuhusu jinai za Israel katika vita vya Gaza

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Alkhamisi wiki hii alitoa ripoti yake kuhusu vita vya siku 12 vya Israel na mashambulizi ya kikatili ya utawala huo dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Katika ripoti hiyo, Michelle Bachelet ameashiria uhasama unaoongezeka kila siku katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel na kusisitiza kuwa, mikakati ya Israel ya kuwafukuza Wapalestina katika kitongoji cha Sheikh Jarrah na uvamizi wa jeshi la utawala huo dhidi ya Msikiti wa al Aqsa vinachochea zaidi uhasama huo. 

Bachelet pia ameashiria mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya makazi ya raia katika eneo la Ukanda wa Gaza na kusema kuwa: "Israel inadai kuwa, imeshambulia makundi yanayobeba silaha huko Gaza, lakini mashambulizi hayo yameua na kujeruhi raia. Vilevile hatujapata ushahidi wowote kwamba, makundi ya wanamgambo wa Gaza yametumia taasisi na makazi ya raia yaliyoharibiwa kwa mabomu na mashambulizi ya Israel."

Matamshi hayo ya kiongozi wa juu kabisa wa taasisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa yanaweka wazi nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuchochea mapigano ya karibuni baina ya utawala huo na Wapalestina, yaani vizingiti vinavyowazuia Wapalestina kuingia katika Msikiti wa al Aqsa na mikakati ya utawala huo ya kuwafukuza Wapalestina katika eneo la Sheikh Jarrah huko Quds Mashariki, na vilevile uongo wa visingizio vilivyotumiwa na Wzayuni kwa ajili ya kushambulia makazi ya raia wa Gaza katika vita vya siku 12. Mashambulizi hayo ya kikatili yalikuwa makubwa sana ya yamesababisha uharibifu mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa katika eneo hilo mbali na kuua na kujeruhi mamia ya raia wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wadogo. Ahmad  Abuzahri ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema: "Israel ilianzisha vita vya karibuni huko Gaza kwa shabaha ya kushambulia vituo vyote vya kiraia ikiwa ni pamoja na shule, misikiti, nyumba za raia na taasisi za serikali, na mashambulizi hayo yamekabiliwa na jibu kali la wanamapambano na taifa la Palestina."

Jengo la wa waandishi wa habari la al Jalaa lililoshambuliwa na Israel, Gaza

Udhaifu wa hoja na visingizio vilivyotumiwa na Wazayuni kuhalalisha mashambulizi dhidi ya makazi ya raia kwa madai kwamba, harakati za mapambano za Palestina zilificha silaha katika majengo ya raia, umedhihirika vyema zaidi katika ripoti ya Michelle Bachelet. 

Suala jingine lililowekwa wazi na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ni kwamba, eneo la Ukanda wa Gaza limekuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani. Katika miaka ya karibuni Israel imekuwa ikifanya ukatili na mashambulio ya kinyama huko katika Ukanda wa Gaza na kuua raia na kuharibu miundombinu na nyumba za raia. Israel pia inalizingira eneo hilo linalotambuliwa kuwa na msongamano mkubwa wa watu tangu mwaka 2007. Vitendo hivyo vya Israel vinatambuliwa kuwa ni kielelezo cha jinai dhidi ya binadamu.

Baada ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha ripoti yake kuhusu ukatili na jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeafiki kuunda tume ya kimataifa ya kufanya uchunguzi kuhusu jinai hizo. Inaonekana kuwa, kuundwa na kuanza kazi tume hiyo kutafichua na kuweka wazi zaidi uhalifu na jinai kubwa zilizofanywa na utawala katili wa Israel katika maeneo mbalimbali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuufedhehesha zaidi utawala huo na madola ya Magharfibi yanayowahami na kuwakingia kifua Wazayuni makatili hususan Marekani.

Mshikamano wa kimataifa dhidi ya Israel ulioonekana katika kalibu na sura ya kuundwa tume ya kuchunguza jinai za kivita na dhidi ya binadamu za utawala huo ghasibu huko Gaza, umewakasirisha sana viongozi wa Tel Aviv na washirika wao wa Kimagharibi. Balozi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa, Gilad Erdan, amelaani hatua ya Baraza la Usalama ya kupasisha muswada wa kuundwa tume ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Israel huko Ukanda wa Gaza na amelituhumu Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuwa linawapiga vita Wayahudi!

Watoto wa Gaza.... 

Hata hivyo tuhuma hizo zisizo na msingi hasa tabia ya Israel ya kuitumia vibaya Marekani katika madai eti ya "chuki dhidi ya Mayahudi" zimepitwa na wakati, na sasa walimwengu wametambua vyema jinai na uhalifu usio na kifani unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina kupitia ripori na matangazo ya vyombo vya habari na miandao ya kijamii; hivyo Israel haitakuwa tena na fursa ya kendelea kujidhihirisha mbele ya walimwengu kama taifa lililodhulumiwa na kujiliza machozi ya mamba mbele ya vyombo vya habari.     

Tags