May 16, 2016 06:54 UTC
  • Trump: Wakimbizi wa Syria wanapanga shambulizi kama la Septemba 11

Donald Trump, mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Republican nchini Marekani kwa mara nyingine tena ametoa matamshi yanayodhihirisha misimamo yake ya chuki na ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na wageni. Trump amedai kuwa wakimbizi wa Syria nchini Marekani wanapanga njama ya kufanya shambulizi la kigaidi kama la Septemba 11.

Trump amedai kuwa lazima Marekani itashuhudia mashambulizi mengine ya kigaidi kama lile la Septemba 11 mwaka 2001, kutoka kwa wakimbizi wa Syria wanaopewa hifadhi katika nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo mbaguzi amesema na hapa tunanukuu: "Mambo mengi mabaya yatafanyika nchini, sina shaka kwamba mashambulizi mengi ya kigaidi yatafanyika, yote haya yatasababishwa na kuruhusu wakimbizi wa Syria kumiminika katika nchi yetu," mwisho wa kunukuu.

Trump ambaye amekuwa akikosoa siasa za kigeni za nchi hiyo na kuzitaja kuwa ni msiba mkubwa na zilizokosa mwelekeo au mwanga wa stratijia amedai kuwa, wakimbizi hao hawafai kuruhusiwa nchini humo na kwamba kuwaruhusu ni kuiwekea Marekani katika hatari ya kushuhudia shambulizi jingine kama la Septemba 11 mwaka 2001, ambapo zaidi ya watu 3,000 waliuawa.

Wachambuzi wa siasa za Marekani na hata baadhi ya wanachama wa Republican wamekuwa wakiyakosoa matamshi ya chuki na kibaguzi ya Trump na kusisitiza kuwa, si tu kuwa yanahatarisha usalama wa Marekani pekee bali wa dunia nzima kwa ujumla. Mbali na kuwahi kusema kuwa Waislamu wanapasa kuzuiwa kuingia Marekani eti kwa kuwa ni magaidi, mwanasiasa huyo bilionea amekuwa akitoa kauli za chuki dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Tags