Jun 26, 2021 15:01 UTC
  • Tsunami ya kujiua katika jeshi la Marekani, nembo ya mgogoro wa kinafsi na kimaadili

Ripoti ya karibuni ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) inaonesha ongezeko la visa vya kujiua kati ya wanajeshi wa nchi hiyo hususan maveterani wa jeshi.

Ripoti hiyo inasema zaidi ya maveterani elfu 45 wa jeshi la Marekani au watu waliohudumu katika jeshi katika kipindi cha miaka sita iliyopita wamejiua na kutoa uhai wa wenyewe. Kwa kutilia maanani hali hiyo ya kutisha, Pentagon imetangaza kuwa, inalipa kipaumbele suala la kuchunguza sababu na njia za kuzuia vitendo vya kujiua wanajeshi wa Marekani.

Ripoti mpya pia imetahadharisha kuhusu athari mbaya za kijamii za kujiua wanajeshi wa Marekani hususan kwa kutilia maanani kwamba, wimbi kubwa la kujiua sasa limeingia katika familia za wanajeshi.

Utafiti mpya umefichua kuwa, idadi ya askari wa Marekani na maveterani wa jeshi wa nchi hiyo wanaoaga dunia kwa kujitoa uhai ni mara nne zaidi ya wanajeshi wa dola hilo la kibeberu wanaouawa vitani katika vita vinavyoanzishwa na Washington kila uchao tokea Septemba 11 mwaka 2001.

Carol Giacomo ambaye ni mwandishi wa habari na mtaalamu wa masuala ya siasa anasema: "Wanajeshi 20 wa Marekani hujitoa uhai kila siku inayokwenda kwa Mungu na suala hili linaonesha kuwa idadi ya wanajeshi wanaopoteza maisha yao kwa njia hiyo ni kubwa zaidi kuliko wanajeshi wa Marekani waliouawa katika vita vya Iraq na Afghanistan."

Maelfu ya wanajeshi wa marekani wamejiua wenyewe tangu baada ya Septemba 11, 20001

Inaonekana kuwa, suala hilo la kujiua kwa wingi wanajeshi wa Marekani hususan wale walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq ni miongoni mwa matunda ya vita visivyo na ukomo vya watawala wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya dunia kwenye miongo miwili iliyopita. Vita vya mara kwa mara vilivyoanzishwa na watawala wa White House baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 vimezidisha vitendo vya kujitoa uhai baina ya wanajeshi wa nchi hiyo. Tunaweza pia kusema kuwa, takwimu zilizotolewa na Pentagon kuhusu wanajeshi wa Marekani wanaojitoa uhai wao wenyewe zinaonesha sehemu ndogo sana na matatizo ya kinafsi yanayowasumbua wanajeshi wengi wa nchi hiyo walioshiriki vita vya Iraq na Afghanistan ambao wameathirika sana kiakili na kinafsi. 

Vita vya Marekani nchini Afghanistan vimeisababishia nchi hiyo hasara ya dola Trilioni mbili na bilioni 400. Vilevile tangu Marekani ilipoishambulia na kuivamia ardhi ya Afghanistan miaka 20 iliyopita zaidi ya wanajeshi wake 2,400 wameuawa katika nchi hiyo na maelfu miongoni mwao wamejeruhiwa.

Baada ya Afghanistan, Marekani iliishambulia Iraq bila hata ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwaka 2003. Wakati wa vita vya Iraq wanajeshi karibu elfu tano wa Marekani waliuawa na maelfu ya wengine walijeruhiwa na kuwa vilema. Tangu wakati huo, Marekani iliweka mbele sera ya vita vya kudumu na visivyo na mwisho, suala ambalo limeendelea kuangamiza roho za wanajeshi wa nchi hiyo na kusababisha matatizo mengi ya kimwili na kinafsi kwa maelfu ya wengine.

Wanajeshi wasiopungua 20 wa Marekani hujitoa uhai kila siku

Mbali na hayo, maelfu ya wanajeshi wa Marekani walioshiriki katika vita vya Afghanistan na Iraq na kuendeleza uvamizi wa Washington katika nchi hizo wanasumbuliwa na aina mbalimbali za matatizo na magonjwa ya kiakili na kinafsi, na pale wanaporejea makwao huonekana kuwa na mienendo ya ajabu na isiyofaa kwa watu wa familia zao na katika jamii na hatimaye huamua kujitoa uhai kwa kujiua wenyewe baada ya kushindwa kustahamili adhabu na matatizo mengi ya kinafsi na kiakili.

Wataalamu wa elimu nafsi wanasema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba wanajeshi wote wa Marekani ambao walishiriki mstari wa mbele wa vita kwa muda wa siku 40 watapatwa na aina mojawapo ya matatizo ya kinafsi na kiroho hadi mwishoni mwa umri wao.

Vifo vinavyotokana na kujiua wanajeshi wa Marekani mbali na kuangamiza familia zao, lakini pia vinasambaratisha moyo na mshikamano wa ndani ya vikosi vya majeshi walivyokuwa wakitumikia. Uchunguzi uliofanyika kuhusu visa hivi vya kujitoa roho wanajeshi wa Marekani unaonesha kwamba, wanajeshi hao waliwahi kuwa katika maeneo ya vita, kukumbwa na sonono, matatizo ya kinafsi, utumiaji mbaya wa dawa na matatizo ya kibinafsi.

Matatizo ya kinafsi ya kiakili ya wanajeshi wa Marekani waliokuwa Iraq na Afghanistan yanasababisha kujiua wao wenyewe.

Baadhi ya wataalamu wa elimu nafsi pia wanasema ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Marekani katika maeneo kama Afghanistan na Iraq na mienendo mibaya ya maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani dhidi ya wale walioko chini yao na kadhalika vimezidisha msongo wa mawazo na mashinikizo ya kinafsi ya wanajeshi hao na hatimaye kujiua wenyewe. Hii ni pamoja na kuwa, baada ya kurejea makwao baadhi ya wanajeshi hao hushindwa kurejea tena katika mazingira ya kawaida na kuanza kuishi katika hali ya mgongano wa kinafsi. Vilevile maveterani wengi wa Marekani wanasumbuliwa na hali mbaya ya kimaisha ambayo mara nyingi huwasukuma upande wa kujitoa uhai.       

Tags