Idadi ya watu waliofariki katika mafuriko yaliyotokea Ulaya imefika 153
Watu 153 wamefariki dunia hadi sasa kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua kali zilizonyesha magharibi na kaskazini mwa Ulaya na kusababisha mito kufurika na kingo zake kupasuka.
Maelfu ya watu katika nchi za maeneo ya magharibi na kaskazini mwa bara hilo wamelazimika kuyahama makazi yao pia, na hadi sasa nyumba nyingi zimebomolewa na mafuriko hayo angamizi.
Nchini Ujerumani pekee, watu wasiopungua 133 wameaga dunia hadi sasa kutokana na janga hilo la mafuriko.
Ubelgiji pia imepata hasara kubwa kutokana na mafuriko kiasi kwamba nyumba nyingi zimebomoka na kusombwa na maji.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ubelgiji ilitangaza jana kuwa, watu 20 wamefariki na wengine 20 hawajulikani waliko.
Mafuriko yamesababisha hasara kadhaa pia katika nchi za Luxemberg, Uswisi na Uholanzi. Ripoti zinaeleza kuwa maelfu ya watu wamehamishwa katika mji wa Maastricht nchini Uholanzi.
Katika mji mkuu wa Uingereza, London pia mvua kali za mafuriko zimewafanya watu walazimike kuzihama nyumba zao na kufungwa njia za mawasiliano…/