Mullah Hassan Akhund apendekezwa na Taliban kuwa rais mpya wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74352-mullah_hassan_akhund_apendekezwa_na_taliban_kuwa_rais_mpya_wa_afghanistan
Baadhi ya vyombo vya habari vya Pakistan vimetangaza kuwa, kundi la Taliban la Afghanistan limempendekeza Mullah Hassan Akhund kuwa rais wa baadaye wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2021 06:01 UTC
  • Mullah Hassan Akhund apendekezwa na Taliban kuwa rais mpya wa Afghanistan

Baadhi ya vyombo vya habari vya Pakistan vimetangaza kuwa, kundi la Taliban la Afghanistan limempendekeza Mullah Hassan Akhund kuwa rais wa baadaye wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya Pakistan vimeongeza kuwa, kiongozi wa kundi la Taliban, Hibatullah Akhundzada amependekeza Muhallah Hassan Akhund kuwa Rais, au Waziri Mkuu au Msimamizi mpya wa serikali ya Afghanistan na Mulla Baradar Akhund na Mulla Abdus Salaam kuwa manaibu wake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi la Taliban limeshamaliza mipango yote ya kutangaza serikali mpya. Serikali hiyo ilikuwa itangazwe rasmi jana Jumatatu lakini kutokana na sababu mbalimbali, zoezi hilo limeakhirishwa. Baadhi ya viongozi wa Taliban wamesema kuwa, kuna uwezekano serikali mpya ya Afghanistan ikatangazwa rasmi kesho Jumatano au ikaakhirishwa tena kwa siku kadhaa.

Hibatullah Akhundzada kiongozi mkuu wa Taliban

 

Hivi sasa Mullah Hassan Akhund ni mkuu wa chombo chenye nguvu zaidi za kuchukua maamuzi ndani ya kundi la Taliban yaani Baraza la Uongozi na ni mmoja wa waanzilishi wa kundi lenye silaha ndani ya Taliban. Ana uzoefu wa kuongoza Baraza la Uongozi la Taliban kwa muda wa miaka 20.

Ikumbukwe kuwa, hadi hivi sasa kundi la Taliban halijapata uungaji mkono wa Waafghani wote. Siku chache zilizopita, Ahmad Masoud, Kiongozi wa Waafghanistan wanaolipinga kundi la Taliban alitoa mwito wa kuendelezwa mapambano dhidi ya kundi hilo. Ahmad Masoud, ambaye ni mwana wa Ahmad Shah Masoud, shujaa wa taifa wa Afghanistan alisema kwamba: "Hatutaacha katu kupambana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, uhuru na uadilifu."