Pakistan yatuhumiwa kuunga mkono na kuisaidia Taliban katika mapigano ya Panjshir
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74376-pakistan_yatuhumiwa_kuunga_mkono_na_kuisaidia_taliban_katika_mapigano_ya_panjshir
Sambamba na kuripotiwa habari zenye kugongana kuhusu kutekwa mkoa wa Panjshir nchini Afghanistan, kambi ya wapinzani katika mkoa huo imeituhumu Pakistan kuwa imeliunga mkono na kulisaidia kundi la Taliban katika mapigano ya eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2021 02:56 UTC
  • Pakistan yatuhumiwa kuunga mkono na kuisaidia Taliban katika mapigano ya Panjshir

Sambamba na kuripotiwa habari zenye kugongana kuhusu kutekwa mkoa wa Panjshir nchini Afghanistan, kambi ya wapinzani katika mkoa huo imeituhumu Pakistan kuwa imeliunga mkono na kulisaidia kundi la Taliban katika mapigano ya eneo hilo.

Wapiganaji wa vikosi vinavyopinga Taliban katika bonde la Panjshir wameituhumu Pakistan kuwa imevipatia misaada ya anga na nchi kavu vikosi vya Taliban ili viweze kuuteka mkoa huo.

Kuhusiana na suala hilo, Ahmad Masoud, kamanda wa wapinzani wa Panjshir ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa twitter akisema: "Si Taliban inayopigana vita na sisi, bali ni jeshi na Shirika la Intelijensia la Pakistan (ISI)."

Ahmad Masoud (katikati) Kamanda wa wapiganaji wa Panjshir

Makamanda wa kijeshi wa wapinzani wa Taliban katika mkoa wa Panjshir nao pia wamesema, ndege zisizo na rubani za Pakistan zimewashambulia wapiganaji wao katika eneo hilo. Aidha duru kadhaa zimedai kuwa, Pakistan si tu inaisaidia Taliban kwa njia ya anga, lakini hata askari wa jeshi la nchi hiyo pia wanalisaidia kundi la Taliban katika operesheni za nchi kavu kwenye vita na wapinzani wa kundi hilo.

Hayo yanaripotiwa huku msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid akidai kupitia ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wa kijamii wa twitter kwamba, mkoa wa Panjshir umeshadhibitiwa kikamilifu na wapiganji wa kundi lao.../