Ripoti: Kanisa Katoliki Ufaransa lina maelfu ya makasisi waliolawiti watoto
Maelfu ya makasisi na maafisa wengine wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa wanakabiliwa na tuhuma za kuwanyanyasa na kuwadhalilisha kingono watoto wadogo.
Jean-Marc Sauve, Mkuu wa Kamisheni Huru ya Uchunguzi inayofuatilia faili la kashfa za makasisi wa Kanisa Katoliki kubakwa na kuwalawitiwa watoto wadogo nchini Ufaransa amesema, kuna makasisi, maaskofu na maafisa wa kanisa hilo kati ya 2,900 na 3,200 waliowadhalilisha kingono watoto wa kike na wa kiume katika nchi hiyo ya Ulaya tokea mwaka 1950.
Sauve ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, idadi hiyo tajwa ni makisio ya kiwango cha chini kabisa; na kwamba ripoti hiyo inatazamiwa kutoa mapendekezo 45.
Ripoti hiyo yenye kurasa 2,500 na inayotazamiwa kutolewa rasmi Jumanne ijayo, imekosoa vikali kuruhusiwa kuendelea kuhudumu makasisi hao wa Kikatoliki nchini Ufaransa, licha ya kuandamwa na sakata hilo la ufuska.
Haya yanaarifiwa miezi michache baada ya uchunguzi wa shirika la habari la Associated Press kufichua kuwa, makasisi, maaskofu, mapadri na maafisa wengine 1,700 wa Kanisa Katoliki nchini Marekani wanaishi huru bila kufuatiliwa na vyombo vya sheria, licha ya kukabiliwa na tuhuma za kuwadhalilisha kingono mamia ya watoto wadogo.
Kuna mamia ya kesi za ubakaji na ulawiti zinazowakabili makasisi wa kanisa hilo, ambazo zimerundikana katika mahakama za Ulaya na Marekani zikisubiri kufanyiwa uchunguzi, jambo ambalo limeshusha hadhi ya Kanisa Katoliki duniani.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis anatafakari kuhusu uwezekano wa kuwaruhusu makasisi, maaskofu, mapadri na watawa wa kanisa hilo waoe na kuolewa kwa wale wanaotaka, kinyume kabisa na kanuni ya kihafidhina ya kanisa hilo.