Lavrov: Kuna tishio la kigaidi huko Idlib, Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa kuna tishio la kigaidi katika mkoa wa Idlib kaskazini mwa Syria na kwamba tishio hilo linaongezeka pia katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenzake wa Misri, Sami Shoukry, Sergei Lavrov alisisitiza ulazima wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kueleza kuwa, makundi ya kigaidi yanaendeleza mashambulizi katika mkoa wa Idlib kaskazini mwa Syria. Amesema makundi hayo ya kigaidi yanapasa kusambaratishwa haraka iwezekanavyo.
Lavrov amesisitiza katika kikao hicho na waandishi wa habari kuwa, njia ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria inapasa kupatikana ili kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza pia ulazima wa kufanyika uchaguzi huko Libya na kueleza kuwa, wanajeshi wote wa nchi ajinabi wanapasa kuondoka nchini humo.
Kwa upande wake Sami Shoukry Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesisitiza kuwa kuna udharura wa kuisaidia Syria ili iondokane na mgogoro wa sasa na kwamba ipo haja ya kutekeleza kikamilifu maazimio ya kimataifa kuhusu nchi hiyo na kuchukuliwa hatua za kulinda amani na usalama nchini humo.
Syria katika miaka ya karibuni imeathiriwa na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na makundi yanayoungwa mkono wa nchi za Magharibi na za Kiarabu ambayo hadi sasa yameua maelfu ya Wasyria na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.