Shule zafungwa Delhi, India kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa
Shule zote katika mji mkuu wa India, New Delhi zimefungwa kutokana na hali chafu ya hewa.
Kamisheni ya Kusimamia Usafi wa Hali ya Hewa nchini India imesema taasisi zote za elimu nchini humo kuanzia jana Jumatano zitafungwa kwa muda usiojulikana, hadi taarifa mbadala itakapotolewa.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu kiwango cha usafi wa hewa katika miji mikubwa duniani zinaonesha kuwa, mji mkuu wa India, New Delhi ndio wenye hewa chafu zaidi duniani.
Ripoti ya jarida la Lancet ya mwaka jana inaonesha kuwa, watu 17,500 waliaga dunia jijini Delhi kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa mwaka juzi 2019.
Januari mwaka huu, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kuwa, watu zaidi ya milioni saba hufariki dunia kila mwaka duniani kote kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa.