Kiongozi mpya wa Ujerumani aanza kazi kwa kuitisha Russia
Kansela mpya wa Ujerumani Olaf Scholz, ambaye amechukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo kutoka kwa Angela Merkel, ameanza kazi kwa kutoa vitisho dhidi ya Russia.
Akijibu mwaswali ya waandishi habari Jumatano katika siku yake ya kwanza ya kazi, Kansela Scholz amedai kuwa, iwapo Russia itaishambulia Ukraine, basi Ujerumani itatafakari kufunga bomba la gesi la Nord Stream 2 ambalo linaingiza gesi ya Russia barani Ulaya.
Ujerumani inatoa vitisho dhidi ya bomba linalofikisha gesi ya Russia barani Ulaya katika hali ambayo wakuu wengi wa nchi za Ulaya wamekuwa wakidai kuwa wana wasiwasi kuwa, Russia itatumia bomba hilo ya gesi kushinikiza nchi zao.
Hivi karibuni viongozi wa Ukarine na Ulaya magharibi wamezidisha propaganda zao dhidi ya Russia na kudai kuwa eti Russia imeongeza askari wake katika mpaka wa Ukraine na hivyo ni dalili ya kukaribia kuvamia Ukraine.
Russia imesisitiza kuwa kutuma askari wake katika mpaka na Ukraine ni hatua ya kawaida ya kijeshi lakini Marekani na waitifaki wake wanataka kuonyesha kuwa kuna hali ya taharuki katika mpaka wa Russia na Ukraine.
Jana Jumatano, serikali mpya ya muungano nchini Ujerumani ikiongozwa na Olaf Scholz wa chama cha Social Democratic - SPD iliapishwa kuchukua usukani mjini Berlin, na kuhitimisha muhula wa miaka 16 wa utawala kansela Angela Merkel katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.
Kansela Scholz anatazamiwa kukutana na mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO Jens Stoltenberg Ijumaa jioni ambapo kadhia ya Russia inatazamiwa kutawala ajenda ya kikao hicho.