Radiamali ya Taliban kwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan
Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa serikali ya Taliban ametoa radiamali kwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Pakistan akisema kuwa: Hakuna mtu atakayeruhusiwa kutumia ardhi ya Afghanistan dhidi ya mataifa mengine.
Amir Khan Motaqi amesema kinagaubaga kwamba, hakuna tishio lolote kutokea katika ardhi ya Afghanistan, lakini kama makusudio ya Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan ni kwamba, serikali dhaifu nchini Afghanistan haiwezi kukabilianba na vitisho, hiyo ni mada nyingine ya kando na sisi tuna matarajio jambo kama hilo lisitokee. Waziri Mkuu wa Pakistan alisema Jumapili iliyopita katika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu {OIC) mjini Islamabad kwamba: Kundi la kigaidi la Daesh linatumia ardhi ya Afghanistan kwa ajili ya kutekeleza operesheni za kigaidi dhidi ya Pakistan, na kwamba kama serikali ya Taliban haitaimarishwa, basi haitakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto hiyo.
Matamshi ya Imaran Khan kuhusiana na kundi la Daesh kuitumia ardhi ya Afghanistan kwa ajili ya kutekeleza hujuma na mashambulio ya kigaidi dhidi ya Pakistan daima yamekuwa yakitumiwa kama fimbo dhidi ya serikali ya Kabul hata kabla ya kuingia tena madarakani wanamgambo wa Taliban. Kwa mtazamo wa serikali ya Pakistan ni kuwa, hali ya ukosefu wa uthabiti nchini Afghanistan imeandaa uwanja wa kuingia nchini humo makundi mbalimbali ya kigaidi likiwemo la Daesh na kundi hilo linaitumia ardhi ya Afghanistan kwa ajili ya kupanga na kutekeleza hujuma na mashambulio yake dhidi ya Pakistan.

Licha ya kuweko utendaji wa namna hii nchini Pakistan, lakini serikali ya Taliban imesisitiza mara chungu nzima juu ya kufanya mambo katika fremu ya mkakati wa kujenga na kuleta hali ya kuaminiana baina ya mataifa ya eneo la Asia Magharibi hususan Pakistan, na kwamba, haitaruhusu ardhi ya Afghanistan igeuzwe na kuwa ngome ya kutekeleza njama za uharibifu dhidi ya mataifa mengine.
Kwa kuzingatia siasa za miezi ya hivi karibuni za Pakistan za kuiunga mkono serikali ya Taliban nchini Afghanistan, matamshi ya Imran Khan katika kikao cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu {OIC} huko Islamabad hayapaswi kutathminiwa kama ukosoaji wake kwa utendaji wa serikali ya Taliban huko Afghanistan.
Tangu wanamgambo wa Taliban waliposhika hatamu za uongozi nchini Afghanistan Agosti 15 mwaka huu {2021} Pakistan imetoa himaya na uungaji mkono mkubwa zaidi kwa kundi hilo na katika miezi ya hivi karibuni sanjari na kusisitiza udharura wa jamii ya kimataifa kuisaidia Afghanistan ili ivuke kipindi hiki cha mgogoro wa sasa imekuwa ikifuatilia suala la kuachiliwa mali na milki za nchi hiyo zinazoshikiliwa na Marekani.

Tangu Taliban itwae madaraka ya nchi baada ya kuanguka serikali ya Rais Muhammad Ashraf Ghani aliyeikimbia nchi, Pakistan imefanya hima kubwa na kutumia nyenzo ilizonazo kwa ajili ya kuthibitisha na kuimarisha nafasi ya wanamgambo hao nchini Afghanistan.
Kufanya mazungumzo na mataifa mbalimbali na kuyataka mara kadhaa madola ya Magharibi yaitambue rasmi serikali ya Taliban kama mtawala mpya nchini Afghanistan ni miongoni mwa juhudi za serikali ya Islamabad zinazolenga kuimarisha nafasi ya wanamgambo hao.
Matamshi ya Imran Khan ya kundi la Daesh kutumia ardhi ya Afghanistan kwa ajili ya kutoa pigo kwa Pakistan kama alivyosema Amir Khan Motaqi, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan ni indhari ya Imran Khan kuhusiana na matokeo mabaya ya kuweko serikali dhaifu nchini Afghanistan.
Kwa maneno mengine ni kuwa, kabla ya Imar Khan kuituhumu Taliban kwa udhaifu katika kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh anataka kutoa indhari na onyo kwa jamii ya kimataifa kwamba, kama serikali ya Taliban haitatambuliwa rasmi na Afghanistan kutopatiwa himaya na uungaji mkono wa kimaada na kinaawi, serikali dhaifu nchini Afghanistan hataiwezi kukabiliana na vitisho kutoka nje.
Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afghanistan akajibu kwa lugha laini matamshi ya Imaran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusiana na hujuma na mashambulio ya Daesh kutoka katika ardhi ya Afghanistan.
Hata hivyo tunapaswa kuzingatia kwamba, licha ya mkakati wa Pakistan wa kutoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa serikali ya Taliban nchini Afghanistan, lakini viongozi wa Islamabad nao wanataraji kuliona kundi hilo katika mazingira ya sasa likitoa radiamali athirifu kuhusiana na kukabiliana na kila aina ya hatua ambayo inatishia amani ya Pakistan kutokea upande wa Afghanistan.