Marekani yaendeleza msimamo ulio dhidi ya makubaliano ya nyuklia, JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i81862-marekani_yaendeleza_msimamo_ulio_dhidi_ya_makubaliano_ya_nyuklia_jcpoa
Mwakilishi maalumu wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran ameendeleza msimamo wa Washington ulio dhidi ya makubaliano ya nyuklia, JCPOA kwa kudai kwamba, serikali ya sasa haiwezi kutoa hakikisho na dhamana juu ya maamuzi yatakayochukuliwa na serikali ijayo ya Marekani kuhusu makubaliano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2022 23:09 UTC
  • Marekani yaendeleza msimamo ulio dhidi ya makubaliano ya nyuklia, JCPOA

Mwakilishi maalumu wa serikali ya Marekani katika masuala ya Iran ameendeleza msimamo wa Washington ulio dhidi ya makubaliano ya nyuklia, JCPOA kwa kudai kwamba, serikali ya sasa haiwezi kutoa hakikisho na dhamana juu ya maamuzi yatakayochukuliwa na serikali ijayo ya Marekani kuhusu makubaliano hayo.

Pasi na kuashiria hatua ya Marekani ya kujitoa kinyume cha sheria katika JCPOA, Robert Malley, mwakilishi maalumu wa serikali ya Washington katika masuala ya Iran amesema, haiwezekani kuihakikishia Iran kwamba serikali ijayo ya Marekani itachukua hatua gani kuhusu JCPOA.

Malley ametoa kauli hiyo, huku Sayyid Kamal Kharrazi, Mkuu wa Baraza la Kistratejia la Uhusiano wa Nje la Iran akisistiza kuwa, kufufuliwa kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuko karibu na kunategemea irada na utashi wa kisiasa wa Marekani.

Licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kukiri kuwa Iran ilikuwa inatekeleza kikamilifu ahadi na majukumu yake yote kuhusiana na JCPOA, serikali ya Marekani wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na Donald Trump, mnamo tarehe 8 Mei, 2018 ilichukua hatua ya upande mmoja ya kujitioa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa yaliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuanzisha kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran.

Katika kile alichodhani kuwa ndio njia ya kufanikisha kampeni yake hiyo, Trump si tu alivirejesha tena vikwazo vyote vya nyuklia vilivyokuwa vimesitishwa dhidi ya Iran, lakini alitekeleza pia vikwazo vingine vipya dhidi ya Tehran.

Baada ya Joe Biden kuingia madarakani, serikali mpya ya Marekani ilikiri kuwa sera ya vikwazo vya juu kabisa iliyotekelezwa na Trump imegonga mwamba na kwamba nchi hiyo inataka kurudi tena kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hata hivyo hadi sasa Washington imekataa kutekeleza hatua zinazotakiwa ili kuweza kujiunga tena na makubaliano hayo.../