May 30, 2022 11:02 UTC
  • Umoja wa Ulaya washindwa kuiwekea Russia vikwazo vya mafuta; hitilafu zaongezeka

Jitihada za Umoja wa Ulaya za kufikia muafaka kuhusu kutekeleza awamu ya sita ya vikwazo dhidi ya Russia zimegonga mwamba kwani Hungary ni moja ya wapinzani wakubwa zaidi wa mpango huo. Wanadiplomasia wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya katika kikao chao maalumu cha Jumapili walijadili mpango wa kuzuia meli za mafuta za Russia kuingiza mafuta Ulaya lakini waruhusu mafuta hayo yaingie kwa mabomba. Hata hivyo mazungumzo hayo yalimalizika bila natija.

Kwa mujibu wa pendekezo la hivi karibuni, Hungary, Slovakia na Jamhuri ya  Czech zilikuwa zipate idhini ya kuendelea kununua mafuta kutoka Russia kwa kutumia bomba la mafuta lijulikanalo kama Druzhba ambalo linapitia Ukraine na ambalo lilijengwa wakati wa zama za Shirikisho la Sovieti. Kuidhinisha uuzaji wa mafuta ya Russia kwa baadhi ya nchi za Ulaya kunamaanisha  kuwa robo moja ya mafuta ya Russia yanayouzwa Ulaya yataondolewa vikwazo na hivyo Moscow itaendelea kupata fedha ambazo Wamagharibi, hasa Wamarekani, wanafanya juu chini isizipate.

Ursula von der Leyen Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya wiki kadhaa zilizopita alipendekeza kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka 2022 ununuzi wa mafuta ya petroli kutoka Russia utakuwa ni marufuku. Hata hivyo kutokana na hitilafu zilizopo baina ya nchi za Ulaya inalekea kuwa itakuwa vigumu sana kupiga marufuku kikamilifu ununuzi wa mafuta ya Russia.

Hungary ni moja ya nchi zinazopinga vikali pendekezo la kupigwa marufuku mafuta ya Russia kwa sababu inategemea sana mafuta hayo. Aidha wakuu wa Hungary wanasema iwapo wataacha kununua mafuta ghafi ya petroli kutoka Russia watalazimika kubadilisha muundo wa viwanda vya kusafisha mafuta na mpango kama huo utagharimu mabilioni ya Euro na utachukua muda wa miaka mitano.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Mihály Orbán ametajwa kuwa kizingiti kikuu katika kutekelezwa mpango huo wa kupiga marufuku mafuta ya Russia.

Suala hilo limeibua mgogoro mkubwa baina ya Hungary na waitifaki wake wa jadi Ulaya ya Kati.  Upinzani wa Hungary unamaanisha kusitishwa awamu zote za vikwazo dhidi ya Russia kama vile kushadidisha vikwazo vya benki na kuzuia meli za Russia na pia kuwawekea vikwazo vya usafari makumi ya maafisa wa ngazi za juu wa Ruusia.

Kwa kuzingatia kutofikiwa mapatano katika kikao cha wanadiplomasia wa Ulaya Jumapili, sasa inatazamiwa kuwa kadhia hiyo itajadiliwa katika kikao cha viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana Jumatatu na Jumanne mjini Brussels.

Kikao hicho kinatazamiwa kujadili vifurushi vya vikwazo vipya dhidi ya Russia ambavyo vinajumuisha vikwazo vya mafuta ya petroli kwa lengo la kuhakikisha nchi za Ulaya zinaacha kuitegemea Russia katika nishati.

Hivi sasa ni wazi kuwa nchi za Umoja wa Ulaya hazijaafikiana kuhusu vikwazo dhidi ya Russia. Kimsingi ni kuwa nchi zinazotegemea mafuta ya Russia zinaona vigumu sana kununua mafuta kutoka maeneo mengine duniani kwani  yamkini zikapata hasara kubwa kiuchumi. Hungary na Slovakia zinasisitiza kuwa kupiga marufuku mafuta ya Russia ni jambo ambalo litavuruga uchumi wa Ulaya. Kwa hivyo Umoja wa Ulaya sasa una machaguo mawili, chaguo la kwanza ni kuzingatia maslahi yake ya kiuchumi na hivyo kuendeleza ununuzi wa mafuta na gesi kutoka Russia na kwa njia hiyo kuzuia uchumi wake kuharibika. Chaguo la pili ni kuamua kufuata sera za Marekani na malengo jumla ya kisiasa ya nchi za Magharibi yaani kukabiliana na madola makubwa, hasa Russia na China, ambayo yanataka mabadiliko katika mfumo wa sasa wa kimataifa. Chaguo hili la mwisho bila shaka litakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa Ulaya.

Inaelekea kuwa, ingawa Umoja wa Ulaya umeafikiana na Marekani kuhusu kuiwekea Russia vikwazo lakini ni wazi kuwa umoja huo tayari umefeli katika kutekeleza kivitendo vikwazo vya mafuta dhidi ya Moscow.

Hii ni katka hali ambayo Ukraine imekuwa ikishinikiza sana kupitishwa na kutekelezwa vikwazo vya mafuta na kifedha dhidi ya Russia ili Moscow ikumbwe na matatizo katika kugharamia vita vyake huko Ukraine.

Kuendelea hitilafu baina ya nchi za Umoja wa Ulaya kuhusu vikwazo dhidi ya Russia kumepelekea baadhi ya wakuu wa Ulaya kutoa indhari kuhusu matokeo ya hitlafu hizo. 

Ursula von der Leyen Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck amesema,  "baada ya Russia kuivamia Ukraine, tuliona kile kinachoweza kufanyika iwapo Ulaya itadumisha Umoja,...lakini sasa kuna ishara za kusambaratika Umoja wa Ulaya kuliko wakati mwingine wowote ule.

Kimsingi ni kuwa kuna baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya ambazo haziko tayari kutoa muhanga maslahi yao ya kitaifa kwa ajili ya maslahi ya Marekani. Nchi hizo zinaamini kuwa kuendeleza uhasama dhidi ya Russia kutakuwa na madhara makubwa kwa Ulaya katika mtazamo wa kiuchumi, kinishati, na kijeshi.

Tags