Amano: Iran imefungamana na makubaliano ya nyuklia
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) amethibitisha kuwa Iran imefungamana na makubaliano ya nyuklia.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) amesema kuwa kazi ngumu ya kuthibitisha utekelezaji wa ahadi za makubaliano ya nyuklia inachukua miaka kadhaa. Akizungumza katika mahojiano na gazeti la Washington Post, Amano amesema kuwa makubaliano hayo bado yanalegalega na kwamba kufikia muafaka lilikuwa jambo muhimu, hata hivyo akasema ili kuweza kuyalinda makubaliano hayo jitihada chungu nzima zinahitajika. Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amebainisha kuwa, kuidhinisha miradi ya nyuklia ya Iran ni kazi kubwa sana na kwamba wataalamu wa wakala huo wanafanya kazi yao kwa juhudi na weledi wa hali ya juu.
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki Jumatatu iliyopita ulitangaza huko Vienna kuhusu kuanza kikao cha msimu cha Bodi ya Magavana ya wakala huo tarehe sita mwezi huu na kwamba kadhia ya Iran itachunguzwa pia kwenye kikao hicho. Huko nyuma pia Reza Najafi Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika IAEA alieleza kuwa Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo kwa mara nyingine tena amethibitisha kuwa Iran imetekeleza kikamilifu hatua kuhusu miradi yake ya nyuklia kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.