Ripoti: Dunia kushuhudia ongezeko la akiba ya silaha za nyuklia
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imeonya kuwa, akiba ya silaha hatari za nyuklia duniani inatazamiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Katika ripoti yake ya kila mwaka iliyotolewa leo Jumatatu, SIPRI imesema dunia karibuni hivi itashuhudia ongezeko la akiba ya silaha za nyuklia kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tokea enzi za Vita Baridi.
Taasisi hiyo ya kimataifa yenye makao yake nchini Sweden imesema, nchi zote tisa duniani zenye kumiliki silaha za nyuklia ama zinaongeza, au kuboresha silaha zao za atomiki.
Ripoti iliyotolewa na SIPRI imesema kuwa, japokuwa vichwa vya makombora ya nyuklia vinaendelea kupungua kutokana na nchi husika kuharibu vichwa vilivyopitwa na wakati, lakini silaha za nyuklia zinazoweza kutumiwa zimeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Marekani na Russia bado zinamiliki zaidi ya asilimia 90 ya silaha hizo za nyuklia duniani. Russia inaongoza kwa kuwa na vichwa vya makombora ya nyuklia 5,977, huku Marekani ikifuatia kwa vichwa 5,428.
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm imesema japokuwa kuna kuna silaha 12,705 za nyuklia katika maeneo mbalimbali ya dunia, ikilinganishwa na 13,080mwaka jana, lakini kuna uwezekano mkubwa wa vichwa hivyo vikaongezeka kwa kiwango cha kutisha ndani ya miongo kadhaa ijayo.
Mbali na Marekani na Russia, nchi nyingine tatu wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinazozimiliki silaha za nyuklia ni Ufaransa, China na Uingereza. Nchi nyingine zilizorundika silaha za nyuklia ni India, Pakistan, Korea Kaskazini, pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel.