Jul 30, 2022 10:51 UTC
  • Kuendelea ushirikiano wa kiuchumi wa kundi la D-8 katika kikao cha Dhaka

Duru nyingne ya mkutano wa kundi la nchi nane za Kiislamu zilizostawi kiuchumi yaani D-8 imefanyika huku Bangladesh ikiwa mwenyeji wa mkutano huo.

Bangladesh imekabidhiwa duru ya uwenyekiti wa kundi la D-8 katika mkutano uliofanyika kwa njia ya intaneti katika mji mkuu wa nchi hiyo Dhaka. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Pakistan, Malaysia, Indonesia, Bangladesh, Misri na Nigeria ni nchi nane wanachama wa awali wa kundi hilo ambalo limebadilika na kuwa jumuiya. Ukweli ni kuwa, nchi hizi zote zina uwezo na suhula nyingi kama kizazi cha vijana na maliasili mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia kwa kuleta ustawi wa kiuchumi katika Ulimwengu wa Kiislamu. Tangu kuanzishwa kwake, taasisi  ya kiuchumi ya D-8 imekuwa na taathira na ushawishi huku ikidhihirisha misimamo imara dhidi ya ukosefu wa uadilifu na uwepo wa ulimwengu wa kambi moja.  

Kamisheni ya kundi la D-8 mjini Dhaka, Bangladesh 

Taasisi ya kundi la nchi nane za Kiislamu zilizostawi kiuchumi D-8 baada ya kupita zaidi ya robo karne sasa imeendelea kuweka katika ajenda yake ya kazi malengo kama kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Ukweli huu wa mambo hauwezi kupuuzwa kwamba nchi wanachama wa kundi la D-8 zina suhula na uwezo mkubwa ambapo sehemu kubwa ya nguvu hii tajwa haitumiki ipasavyo. Hii ni katika hali ambayo, asilimia 15 ya  maliasili yote ya mafuta duniani na asilimia 23 ya akiba yote ya gesi asilia duniani inamilikiwa na nchi wananchama wa jumuiya hii. 

Wakati huo huo, idadi ya watu katika nchi 8 wanachama wa kundi la D-8 inakaribia bilioni moja; na pamoja na kuwa  kiwango jumla cha uchumi wa kifedha wa nchi hizo kinakaribia dola bilioni elfu 4, lakini kiwango cha ubadilishanaji wa kibiashara kati ya nchi wanachama ndani ya kundi hilo ni cha dola zipatazo bilioni 110; kiwango ambacho kinatajwa kuwa cha chini sana.  Kwa hiyo, nchi za D-8 zinapasa kuzidisha mabadilishano ya kibiashara ya ndani ya nchi zao zenyewe kwa kiwango cha juu zaidi. Kuhusiana na suala hili, Muhammad Ali Basiri mhadhiri wa Chuo Kikuu na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi anaamini kuwa, nchi za D-8 zina azma na irada kuu kwa ajili ya kuimarisha na kuzidisha uhusiano wa kiuchumi kati yazo hata hivyo kwa upande wa utekelezaji, kunashuhudiwa hitilafu kubwa kati ya wanachama katika sekta ya kiuchumi na miundo ya kisera inayoongoza katika nchi hizo; na hili na matatizo mengine hadi sasa yanakwamisha mafanikio ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo."

Weledi wa mambo wanasema kuwa, kuimarishwa kadiri inavyowezekana nafasi ya dini Tukufu ya Kiislamu miongoni mwa nchi wanachama wa kundi la D-8, kushirikiana nchi wanachama ili kutimiza malengo ya kiuchumi ya kundi hilo kupitia kunufaika na suhula na nyenzo kubwa za kila nchi, ushirikiano wa nchi hizo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, nchi wanachama kustafidi na tajiriba miongoni mwao ili kuondoa masuala yote yanayokwamisha ustawi wa kijamii na kiuchumi na kukabiliana na vitisho na changamoto za kimataifa ni miongoni mwa njia ambazo kundi la D-8 linaweza kustafidi nazo ili kuondokana na changamoto zinazolikabili.

Kama wanavyoamini baadhi ya weledi wa mambo, Iran na Uturuki ambazo zilikuwa katika mstari wa mbele katika kuasisiwa taasisi hii muhimu zimelipa umuhimu suala la kuimarisha na kupanua ushirikiano kati ya nchi wanachama wa D-8; na katika suala la utandawazi, taasisi hii inapasa kupewa hadhi yake kimataifa na kutambuliwa kama jumuiya ya kimataifa yenye taathira na nguvu. 

Wakiashiria kuhusu ukweli huu kwamba kundi la D-8 ni taasisi ya aina yake iliyo na nafasi na nyenzo maalumu miongoni mwa taasisi na jumuiya za kimataifa; weledi hawa wa mambo wanasisitiza kuwa, nchi wanachama wa D-8 taasisi yenye eneo kubwa la kijiografia na inayopatikana katika mabara yote matatu duniani zina suhula muhimu na maliasili ya watu imara; ambapo kutumiwa vyema suhula na maliasili hizi tajwa na mwongozo wao makini kunaweza kusaidia kukuza na kuimarisha maslahi ya pamoja katika mataifa ya Kiislamu.   

Ramani ya nchi wanachama wa kundi la D-8 

 

Tags