New Zealand itaacha kuwa chini ya ufalme wa Uingereza, itajitangaza Jamhuri
Sep 13, 2022 21:42 UTC
Waziri Mkuu wa New Zealand amesema nchi hiyo hatimaye itaacha kuwa chini ya mfumo wa kifalme wa Uingereza na kujitangaza kuwa Jamhuri.
New Zealand, pamoja na nchi zingine kadhaa zilizokoloniwa na Uingereza kama Australia na Canada, ingali inamtambua mfalme wa Uingereza kama mkuu wake wa nchi; na hadi sasa picha ya Malkia wa Uingereza inaendelea kuchapishwa kwenye sarafu na noti za nchi hiyo.
Hata hivyo kwa upande wa Australia, serikali ya nchi hiyo imetangaza kuwa, baada ya kifo cha Elizabeth II, picha ya malkia huyo mwendazake wa Uingereza haitachapishwa tena kwenye noti, na kuanzia sasa, picha za shakhsia maarufu wa nchi hiyo ndizo zitakazochapishwa kwenye noti.
Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa, Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema: New Zealand itamweka pembeni mfalme wa Uingereza kama mkuu wa nchi na itakuwa taifa huru.
Akizungumzia uhuru wa nchi za Pasifiki ya Kusini, Waziri Mkuu wa New Zealand amesema: "nina imani hili litatokea katika uhai wangu, lakini si katika mustakabali wa karibu."
Baada ya kifo cha Elizabeth II, maandamano ya kupinga ufalme yamefanyika katika nchi nyingi za Jumuiya ya Madola kama vile baadhi ya nchi za Karibea na Pasifiki Kusini, Australia, New Zealand na Canada; na mamlaka ya nchi hizo zinatathmini msimamo wa kumtambua Mfalme Charles III kama kiongozi mkuu wa nchi au kujitenga na Uingereza na kuwa nchi zenye mfumo wa Jamhuri.../
Tags