Sep 25, 2022 02:12 UTC
  • Upinzani wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la Marafiki wa Kutetea Hati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya vikwazo vya upande mmoja

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la Marafiki wa Kutetea Hati ya Umoja wa Mataifa wamedhihirisha upinzani wao dhidi ya vikwazo vya upande mmoja, na kusisitiza juu ya kuheshimiwa mamlaka, ardhi na kujitawala kwa nchi huru. Mawaziri hao wamesisitiza hilo katika mkutano wao uliofanyika kando ya kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 22 huko New York.

Katika kikao hicho, Reza Najafi, Naibu Waziri Wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia Masuala ya Sheria za Kimataifa amesisitiza juu ya kuzingatiwa kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa na kupinga vikwazo vya upande mmoja na visivyo halali vya Marekani dhidi ya Iran.

Kundi la Marafiki wa Kutetea Hati ya Umoja wa Mataifa, linalojumuisha nchi 19, ikiwemo Iran, liliundwa mwaka uliopita wa 2021 kwa ajili ya kukabiliana na ukiukwaji wa mara kwa mara wa kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa unaofanywa na nchi za Magharibi na haja ya kuzingatiwa kanuni hizo.

Taarifa ya mwisho ya mkutano huo iliangazia kupingwa vikwazo vya upande mmoja na athari mbaya za vikwazo hivyo katika kuzidisha njaa, umaskini na uhaba wa chakula duniani. Pia ilisistiza haja ya kuheshimiwa mamlaka za nchi, umoja wa ardhi, kujitawala nchi huru, kuheshimiwa na kutekelezwa kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa na vile vile kuonyesha mfungamano na nchi zinazokabiliwa na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Suala la vikwazo vya upande mmoja vinavyotekelezwa na kambi ya Magharibi hususan Marekani dhidi ya nchi pinzani au zinazopinga ubeberu wa Magharibi limepata umuhimu maradufu katika miaka ya hivi karibuni. Mifano miwili muhimu ya suala hilo ni kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi iliyotumiwa na utawala wa Trump dhidi ya Iran baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018, na ambayo bado inatekelezwa na utawala wa Biden, pamoja na utekelezaji wa vikwazo vikubwa zaidi vya upande mmoja vya kambi ya Magharibi dhidi ya Russia kwa kisingizio cha mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya Ukraine.

Kimsingi, vikwazo vya upande mmoja vinatumiwa na kambi ya Magharibi kama silaha ya mashinikizo dhidi ya nchi nyingine pinzani. Marekani ndiyo mpeperushaji mkuu wa bendera wa vikwazo vya upande mmoja, haramu na kandamizi dhidi ya nchi nyingine ulimwenguni.

Nchi hiyo ya Magharibi inachukuliwa kuwa nchi kubwa zaidi duniani inayotumia vikwazo mbalimbali dhidi ya mataifa mengine huru kwa lengo la kulinda maslahi yake katika pembe tofauti za dunia. Licha ya Marekani kutekeleza vikwazo hivyo dhidi ya nchi nyingine hasa hasimu wake kwa sababu mbalimbali za kisiasa, kibiashara, kiusalama na hata haki za binadamu, lakini tukiachilia mbali sababu za kidhahiri za vikwazo hivyo, jambo lililo wazi ni kuwa sababu kuu ya vikwazo hivyo ni kufuatilia na kulinda maslahi ya Washington ulimwenguni.

Mbali na Iran kuwekewa vikwazo vikali zaidi katika historia ya Marekani na katika fremu ya kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi, lakini nchi hiyo hiyo ya Magharibi imekuwa ikitekeleza vikwazo vingine vya upande mmoja dhidi ya nchi kama vile Russia, China, Venezuela, Cuba, Syria na Korea Kaskazini. Alexander Nova", Naibu Waziri Mkuu wa Russia, anasema: "Dunia nzima imechoshwa na vikwazo visivyodhibitiwa vya Marekani dhidi ya nchi mbalimbali ambazo viongozi wake hawakubaliwi na Washington."

Washirika wa Washington wa bara Ulaya, hasa Uingereza, pia wanashirikiana kwa karibu na Marekani katika kuziwekea vikwazo nchi tofauti ulimwenguni. Vikwazo hivyo hutekelezwa kwa visingizio vya nchi hizo kupinga siasa na hatua za Marekani na Magharibi au kwa madai ya nchi zilizowekewa vikwazo kuhatarisha maslahi ya Magharibi.

Umoja wa Mataifa pia umekosoa mara kwa mara vikwazo hivyo vya upande mmoja vya Marekani, hasa wakati wa janga la virusi vya corona na ugonjwa wa Covid-19, ambapo ulitaka kufutwa au kupunguzwa kwa vikwazo hivyo ili kuziwezesha nchi zilizowekewa vikwazo kufikia kirahisi vifaa muhimu vya matibabu na dawa. Elena Dohan, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu taathira mbaya za hatua za upande mmoja anasema: Vikwazo vya upande mmoja vinadhoofisha mamlaka ya Umoja wa Mataifa na kusababisha hofu katika uga wa ushirikiano wa kimataifa na utawala wa sheria.

Marekani hutumia vibaya Baraza la Usalama kufikia malengo yake maovu duniani

Inaonekana kwamba kutokana na athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na Magharibi, ni lazima kuwepo mwelekeo wa kuimarishwa umoja kati ya nchi zilizowekewa vikwazo, ikiwa ni pamoja na kuundwa muungano wa kimataifa dhidi ya vikwazo hivyo, ili Wamagharibi walazimike kutafakari upya mienendo yao katika uwanja huo. Kuhusiana na hilo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la Marafiki wa Kutetea Hati ya Umoja wa Mataifa katika taarifa yao ya mwisho  ya mkutano huo, wamelaani vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi na kusisitiza ulazima wa kukabiliana kimataifa na vikwazo hivyo vinavyoyasababishia madhara mengi mataifa ya dunia.

Tags