UN yakosoa kuzuiliwa wakimbizi katika nchi za Ulaya
Umoja wa Mataifa umeelezea wasi wasi kuhusu habari za kuzuiliwa wakimbizi wakiwemo watoto wadodo katika mazingira ya kutisha barani Ulaya.
Akiongea mjini Geneva nchini Usiwisi hii leo, Zeid Ra'ad al-Hussein, Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema kuwa, sehemu kubwa ya wakimbizi waliongia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean na nchi za Balkan wanazuiliwa kwenye mazingira ya kuogofya katika nchi za Ulaya na haswa Ugiriki na Italia. Amesema kinachosikitisha zaidi ni idadi kubwa ya watoto walioko katika jela hizo. Mkuu wa Kamisheni Kuu ya Kutetea Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za Ulaya kutafuta njia mbadala ya kuwazuilia watoto hao wanaoandamana na wazazi wao wakimbizi huku akiziasa asasi husika za Umoja wa Ulaya kuharakisha mchakato wa kuwapa hifadhi watoto hao. Aghlabu ya wakimbizi hao ni wananchi wanaokimbia mashambulio ya magenge ya kigaidi haswa katika nchi ya Syria na baadhi yao wanatokea katika nchi za Afrika.
Zaidi ya wakimbizi 208,000 wameingia barani Ulaya tangu mwanzoni mwa mwaka huu wakitumia Bahari ya Mediterranean huku 2,850 miongoni mwao wakifa maji.