Mwanafalsafa: Dunia ipo katika ncha ya kutumbukia kwenye tatizo lisilotatulika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93164-mwanafalsafa_dunia_ipo_katika_ncha_ya_kutumbukia_kwenye_tatizo_lisilotatulika
Mwanafalsafa mashuhuri wa Marekani ameonya kuwa, dunia ipo katika ncha ya kutumbukia kwenye uhabaribifu na janga kubwa ambalo litakuwa muhali kulirekebisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2023 04:08 UTC
  • Mwanafalsafa: Dunia ipo katika ncha ya kutumbukia kwenye tatizo lisilotatulika

Mwanafalsafa mashuhuri wa Marekani ameonya kuwa, dunia ipo katika ncha ya kutumbukia kwenye uhabaribifu na janga kubwa ambalo litakuwa muhali kulirekebisha.

Noam Chomsky amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya Russia Today na kueleza kuwa, kadri siku zinavyopita, ndivyo hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani inazidi kuwa kubwa na wazi. 

Chomsky ambaye ni Profesa Mwandamizi wa Isimu katika Chuo Kikuu cha Arizona ameeleza bayana kuwa, uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia duniani haujawahi kuwa mkubwa kiasi hiki tangu vilipomalizika vita baridi. 

Kadhalika mwanafikra huyo mashuhuri wa Marekani ameionya jamii ya kimataifa kuhusu taathira hasi za kuendelea kupuuza suala la kulinda hali ya hewa na kusisitiza kuwa, kufumbiwa macho hatari za kuharibiwa mazingira kutaiangamiza dunia.

Mwanahistoria huyo mtajika wa Marekani amesema serikali za dunia zimeshindwa kuchukua hatua za makusudi za kuipatia ufumbuzi migogoro hiyo inayotishia jamii ya wanadamu.

Noam Chomsky

Hivi karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilisema kuwa, Marekani inafanya vitimbi ambavyo vinaonesha wazi kuwa lengo lake ni kuichochea Russia itumie silaha za nyuklia.

Aidha mwishoni mwa mwaka uliomalizika, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alionya kuhusu hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani na kusisitiza kuwa, kwamba kosa moja tu la kimahesabu linaweza kuutumbukiza ulimwengu kwenye janga la vita vya silaha za atomiki lisilolipizika.